Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mstaafu Mheshimiwa Mohammed A. Babu ameagwa rasmi jioni ya siku ya uzinduzi wa maadhimisho ya miaka hamsini ya Uhuru mkoani Kagera tarehe 28/11/2011. Tafrija hiyo ya kumuaga mhe. Babu ilikwenda sambamba na ile ya kumkaribisha Mheshimiwa Kanali Mstaafu Fabiani I. Massawe.
Mheshimiwa Mohammed A. Babu ambaye ameitumikia serikali takribani miaka 40, ameweka rekodi ya kuwa kiongozi ambaye ameutumikia mkoa wa Kagera vipindi viwili tofauti akiwa mkuu wa mkoa mwaka 1996 hadi 1999 na kipindi cha mwisho ambacho amemaliza na kustaafu ni kuanzia mwaka 2009 hadi 2011.
Akiwaasa watumishi wa umma katika sherehe hizo Mhe. Babu alisisitiza sana waliokuwa watumishi wa ofisi yake pamoja na watumishi wote wa umma kuzingatia kanuni, taratibu za kazi pamoja na nidhamu katika sehemu zao za kazi. Pia Mhe. Babu aliwasisitiza sana watumishi kujiendeleza kielimu ili kuenendana na wakati na ushindani na ufanisi wa kutekeleza majukumu yao ya kazi.
Aidha, mheshimiwa Babu aliwashukuru waliokuwa watumishi wa ofisi yake kwa kumpa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yake bila matatizo yoyote wakati wote wa kazi zake ofisini. Vile vile aliwashukuru wananchi wa mkoa wa Kagera kwa kushirikiana nae wakati wote wa kazi mpaka anastaafu kama mkuu wa mkoa wa Kagera.
Pia aliwaomba wananchi wote wa mkoa wa Kagera kumpa ushirikiano mkubwa mkuu wa mkoa mpya wa Kagera Mheshimiwa Kanali Mstaafu Fabiani I. Massawe kwa kuwa ni mchapa kazi mzuri na kama atapata ushirikiano mzuri ataweza kuuletea maendeleo makubwa mkoa wa Kagera.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Kagera Mheshimiwa Kanali Mstaafu Fabiani I. Massawe alimshukuru sana Mhe. Babu kwani alimlea akiwa mkuu wa Wilaya ya Karagwe mpaka Mhe. Rais akamuona anafaa na kumteua kuwa mkuu wa mkoa wa Kagera.
Sherehe hizo zilizofanyika katika ukumbi wa Bukoba Club na zilifana sana ambapo zilipambwa na burudani mbalimbali, pia na zawadi mbalimbali zilitolewa na wageni mbalimbali waliohudhuria sherehe hizo kwa Mkuu wa Mkoa Mstaafu Mhe. Babu na Mkuu wa Mkoa Mpya Mhe. Massawe. |