Chimbuko la Kagera day ni haja ya wana –Kagera waishio nje ya mkoa wa Kagera kwa kushirikiana na rafiki zao kutaka kushiriki katika kuendeleza mkoa wetu. Wana- Kagera kwa kutambua jitihada za jamii ya wananchi mkoani Kagera katika kuendeleza mkoa wetu waliona ni busara kwa pamoja wakusanye nguvu ili kuunga mkono jitihada hizo.
Shughuli za Kagera day zilizinduliwa rasmi na Waziri Mkuu wa wakati huo mheshimiwa Edward Lowassa kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, tarehe 28 Novemba 2007. Siku hiyo rasilimali zenye thamani ya shillingi billioni moja na nusu ziliahidiwa au na kutolewa. Timu iliyoandaa shughuli hii ikijumuisha kamati ya Kagera day, viongozi wakuu wa wilaya zote na uongozi wa mkoa walifarijika na kuahidi kuwa utaratibu huu uendelee mpaka ngazi ya mkoa, wilaya, tarafa, kata hata vijiji. Huu ni utaratibu wa wananchi kuhamasishana na kushiriki kwa hiari yao wenyewe katika shughuli za maendeleo.
Ufanisi wa Kagera day ulileta faida ya ziada ambapo wananchi walihamasika na kutaka kushiriki katika shughuli za maendeleo ya mkoa. Mara baada ya shughuli wapo waliohoji kwa nini hawakujulishwa, wengine wakitaka kujua shughuli kama hiyo itafanyika tena lini na wengine kutoa michango hata baada ya siku ya uzinduzi. Lakini pamoja na hilo shughuli za maendeleo kwa mshikamano wa kijamii (si chini ya Kagera day) zilipata nguvu sehemu mbalimbali mkoani kwa wanajamii kukutana kwa hiari na kuchangishana kwa ajili ya ujenzi wa shule.
Mfano; wanajamii ya Ruzinga walikutana mwezi Desemba 2007 na kukusanya rasilimali zinazofikia millioni tatu kusaidia Ruzinga sekondari. Katika mfumo unaoelekea kwenye Kagera day, tarehe 27 August 2008, wanajamii wa kata ya Ibuga walikutana na kuchangia matofari ya kutosha vyumba vinne, mawe tripu 10, mchanga tripu 5, mbao vipande 18, fedha taslimu shillingi 300,000 na ahadi shillingi laki tano.
Somo tunalojifunza katika mifano hiyo hapo juu ni kuwa viongozi wa serikali, watumishi toka sekta mbalimbali na wanajamii wote kwa ujumla wanapata fursa ya kujumuika pamoja. Lengo likiwa kukusanya rasilimali wananchi wanapata fursa ya kutoa lililoko moyoni kuanzia mawazo mpaka rasilimali. Uwepo wa viongozi unaboresha kwa kuondoa dhana potofu katika jamii, kukemea uzembe katika utendaji na kupalilia nia njema hali inayopelekea wananchi kuhamasika na kushiriki kwa nguvu mpya.
Ili shughuli za Kagera day iwe moja ya utamaduni wetu, kamati ya Kagera day/yetu imeandaa utaratibu unaoweza kutumika kuendesha shughuli za namna hii kwa ufanisi katika ngazi ya mkoa, wilaya, tarafa, kata mpaka kijiji. Ni imani yetu kuwa utaratibu huu ukiratibiwa vizuri na kumbukumbu kuwekwa hadharani tutachochea maendeleo ya mkoa wetu kwa kasi zaidi.
NGUVU YA PAMOJA
Kenya wana kauli mbiu ya Harambee, Kiingereza ni fund raising, tunapendekeza kauli mbiu yetu katika ngazi ya mkoa na kwenda chini tuiite nguvu ya Pamoja katika maendeleo, “Nguvu ya pamoja”
Mambo ya kuzingatia katika kutumia nguvu ya pamoja kuleta maendeleo
Lengo/Madhumuni : Kukusanya rasilimali kwa ajili ya kujenga madarasa (zahanati/kisima n.k).
Taasisi husika : Shule ya sekondari.
Mhusika mkuu : Katibu tarafa akisaidiana na diwani wa kata nufaika (tuanze na tarafa)
Kamati ya ufanikishaji : Madiwani wote katika tarafa, watendaji wa kata na vijiji katika tarafa hiyo, wakuu wa shule za sekondari na msingi, wawakilishi toka wilayani, wajumbe toka sekta zenye ushawishi katika eneo.
Ofisa muwajibikaji(accounting officer ): Mkuu wa shule
Kuwa na mtu huyu ni muhimu kwani ataandaa rejista, stakabadhi na orodha ya wahisani amabayo itakuwa wazi kwa wananchi kuihakiki kila wakitaka.
Ufanikishaji wa shughuli
Tarehe ya tukio : Siku ya tukio ipangwe kwa kuepuka shughuli nyingine zinazoweza kuathiri mahudhurio. Ni vema walengwa wakapata taarifa siku 60 kabla ya siku ya siku.
WALENGWA:
Wanajamii kwa ujumla – Ingawa kundi hili michango yao ni kidogo lakini ni muhimu ili kuwajengea utamaduni wa kuchangia shughuli za maendeleo yao kwa hiari. Kuwepo kwao ili kushuhudia ujenga nguvu ya uhamasishaji kwani uondoa mashaka ambacho ni chanzo cha uvumi, uzushi na taarifa za upotoshaji. Pia utoa fursa ya viongozi na wataalamu wanaoelimisha kuwapa wananchi mawazo mapya na kuwaondolea mashaka.
Wachangiaji maalumu : Kutoka katika jamii wapo wanajamii ambao kutokana na moyo wa kupenda maendeleo na uwezo walionao wanaweza kusaidia kukusanya rasilimali. Hawa waainishwe mapema na kutumiwa mialiko. Katika kundi hili ni pamoja na asasi zenye ushawishi kama madhehebu ya dini, hospitali, vyama vya msingi n.k
Wanajamii walioko nje ya eneo : Kundi hili litambuliwe, anwani zao zitafutwe na kamati ifanye mawasiliano nao. Wanapofuatwa kwanza lengo iwe kuwaalika ili wahudhurie na kufanikisha uchangiaji. Kutokana na umbali au shughuli wanaweza kutopata furas ya kufika basi waombwe mchango (taslimu/ahadi).
Bajeti: Bajeti iwe katika makundi manne. Gharama za kuandaa siku ya siku, gharama za siku ya nguvu ya pamoja, gharama za mradi na gharama za kufuatilia ahadi.
Taasisi kubwa/hisani na Watu mashuhuri : Hawa ni watu au taasisi zenye rekodi ya kuchangia maendeleo. Kundi hili ni gumu kulipata lakini kama kuna jinsi ya kuwashirikisha wafuatwe kwani daima donge lao huwa ni nono.
Wataalamu na wahamasishaji : Watambuliwe toka katika jamii au nje wataalamu ambao wanaweza kuzungumzia suala la utamaduni wa kuwekeza katika maendeleo. Pia katika jamii watambuliwe watu waliofanikiwa/wenye ushawishi ili wapewe nafasi ya kuzungumza siku ya siku. Wote hao wapewe agalizo ili mazungumzo yao yalenge kuwahamasisha wanajamii si kuwasimanga au kuwakoga hata kama maneno hayo yatakuwa ndiyo hali halisi waliyonayo. Lakini pia wasidanganywe kwa kuwapa kauli za kuwafariji.
Viongozi: Katika ukusanyaji rasilimali katika ngazi hii waalikwe viongozi toka ngazi ya wilaya na kuendelea juu. Zaidi ni kupata kiongozi ambaye ni mgeni katika eneo husika na awe na rekodi ya kufanikisha shughuli za maendeleo katika eneo lake la kazi. Tunategemea awe mtu mwenye wajibu na uwezo wa kuelezea sera za serikali katika maendeleo akitoa mifano ya ufanikishaji ambayo itakuwa rahisi kwa wananchi kuelewa nakufuata.
UTEKELEZAJI SIKU YA SIKU.
Mialiko kwa walengwa : Walengwa waalikwe mapema kwa barua, kadi, nyumba kwa nyumba (personal selling strategy) na matangazo ya jumla. Kabla ya siku ya siku kamati iwe na idadi yenye uhakika ya mahudhurio kwa asilimia 80. Inapowezekana wawe na dokezo ni rasilimali kiasi gani kwa kiwango cha chini zitachangwa.
Kumbukumbu: Ofisa muwajibikaji awe na vitabu/sitakabadhi kwa ajili ya kutunza kumbukumbu. Iwapo kuna waliokwisha changia basi orodha yao iwekwe tayari kwa ajili ya kuwajulisha wahudhuriaji kama njia moja wapo ya kuwahamasisha.
Mshehereshaji: Awepo mtu anayeweza kuongoza shughuli kwa kuwaelekeza wahudhuriaji katika lengo lililokusudiwa. Ufanikishaji wa lengo na kwa kuzingatia muda ni jambo la muhimu sana .
Burudani : Kwa kuzingatia gharama viwepo vikundi vya burudani. Kwa shughuli ya shule itapendeza kama wanafunzi wataimba nyimbo au tenzi zenye kuihamasisha jamii kuwekeza katika elimu/maendeleo.
Viburudisho : Kwa hadhara iliyodhibitiwa kamati inaweza kuandaa viburudisho kwa waalikwa. Pia sehemu hii nayo inahitaji uangalifu kuepuka kuwa na gharama kubwa zisizowiana na mapato.
Gharama za mradi : Kamati iainishe gharama za mradi mzima na kuchagua sehemu ambayo kwa siku hiyo wangependa walengwa wawasaidie. Nini gharama ya mradi mzima, kipindi cha mradi mpaka kukamilika, vyanzo unavyotegemea kukamilisha mradi na hadhara yako unaiomba ikusaidie wapi/nini? Faida za mradi kwa jamii ni zipi? Hayo ni maswali yanayopashwa kuwekwa wazi kabla ya majibu.
Ukusanyaji wa rasilimali : Uandaliwe utaratibu wa kukusanya rasilimali. Zinaweza kundaliwa fomu za kuchangia, watu wakajaza kwa kusimamiwa na wakaribishaji na wakaja kutambuliwa kwa kusomwa. Njia nzuri zaidi kama kuna muda ni kutambua wafagia uwanja wazuri (pace makers), wawatangulie wenzao bila kuwatisha na taratibu mmoja baada ya mwigine kufuatia kwa kuchangia.
Iwapo kuna taasisi kubwa au watu mashuhuri wenye rekodi ya kuchangia maendeleo utafutwe wakati muafaka katika ratiba ili watoe michango yao . Makampuni ni wazi wangependa kutambulika na hata wanaweza kutaka eneo lote lipambwe taswira yao . Masharti hayo si mabaya kama hakuna mshindani.
Katika kujenga utamaduni wa wanajamii walioko nje ya eneo kujitambulisha na shughuli za maendeleo katika maeneo yao , mtu mwenye ushawishi anaweza kuwapigia simu walengwa wakati wa shughuli na wao wakaahidi toka huko huko waliko. Hii ni njia yenye mafanikio makubwa ila inahitaji maadalizi ya kabla.
Njia nyingine ni kuendesha minada. Wanajamii wanaweza kushirikishwa kwa kuombwa kuleta vitu ambavyo vikiuzwa katika shughuli hiyo fedha zitawekwa katika mfuko. Njia ya pili ni kuuza vitu hivyo kwa mtindo wa kupandisha dau ili atakayeshinda achukue na fedha aliyotamka isaidie mradi. Sawa na mnada wa dau ni mnada wa ongezeko (French style), yaani kila anayetamka anawajibika kulipa tofauti katika ongezeko na wa mwisho anachukua kifaa kinachonadishwa. Hii ni njia nzuri kwani unaweza kununua ng'ombe kwa shillingi elfu moja tu. Hii inawapa fursa washiriki wote kushiriki na kama kuna muda wa kutosha mnaweza kukusanya fedha nyingi sana.
Iwapo utaratibu uliandaliwa vizuri kwa kuwaalika watu, kupokea ahadi/rasilimali inaweza kutafutwa fursa ya kuwatambua hata kama hawakufika. Na kama kuna taarifa nzuri hili liwe jambo la kwanza katika kukusanya rasilimali.
Ratiba : Iandaliwe ratiba itakayowezesha mhusika mkuu akisaidiwa na mshehereshaji kufanikisha lengo. Ratiba lazima izingatie :
-Mapokezi ni jambo muhimu linalomshawishi mlengwa kutoa zaidi. Hii ni pamoja wakati wa kufika, kupokelewa, sehemu ya kukaa na mandhari kwa ujumla. Pia inahusisha muonekano na uchangamkaji wa wakaribishaji.
-Muda wa kuanza na kumaliza shughuli ni muhimu sana. Upangaji wa ratiba uzingatie matumizi ya muda kuepuka upotezaji wa muda mwingi katika tukio moja.
-Uhamasishaji ni jambo muhimu na jukumu hili linaanzia katika mabango kama yapo, hotuba ya kukaribisha hadhara, ujumbe wa wazungumzaji wakuu na vikundi vya burudani. Katika uhamasishaji viongozi na watendaji waeleze bayana ni kwa vipi uwazi utakuwepo katika kukusanya, kutumia na kutoa taarifa kwa wadau wote bila kujali kama walichanga au hapana.
-Ukusanyaji rasilimali ni tukio muhimu katika shughuli nzima hivyo lazima lipewe sehemu nzuri. Tukio hili lifanyike wakati sehemu kubwa ya hadhara imefika na mapema kabla ya watu kuanza kuchoka na kuondoka.
-Taarifa ya makusanyo : Hili ni tukio muhimu. Iwapo hali inaridhisha hadhara ijulishwe kadri ukusanyaji unavyoendelea na bila kukosea lazima mwisho wa shughuli kiasi kilichokusanywa kijulikane.
Nguvu ya pamoja inatakiwa katika kuendeleza mkoa wetu – Kagera yetu.
Kwa nini watu wako tayari kuchangia harusi na misiba lakini si shughuli za maendeleo ?
Sababu kuu ni uwazi wa hali ya juu uliopo katika ukusanyaji wa michango, uwazi katika mipango ya matumizi ya michango inayokusanywa, ushirikishaji wa wachangiaji katika matumizi na taarifa zilizo wazi katika mchakato mzima. Pamoja kuwa na timu ya wahusika wakuu wanaojitoa muda wote kuhakikisha shughuli inafanikiwa. Tuazime uzoefu huu
|