WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS MAHUSIANO NA URATIBU Mhe. STEVEN WASIRA AKAGUA MIRADI YA TASAF MKOANI KAGERA.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu Mhe. Stephen Wasira ametembelea Mkoa wa Kagera na Kukagua miradi inayotekelezwa chini ya TASAF II katika Wilaya ya Muleba. Mhe. Wasira ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayemsaidia Mhe. Rais katika kusimamia na kuhakikisha mahusiano kati ya Serikali na jamii ni mazuri, pia anasimamia Tume ya Mipango ambayo inaratibu Miradi kama TASAF , MKURABITA na miradi mingine ambayo ipo chini ya Tume ya Mipango.
Katika ziara yake Wilayani Muleba Mhe. Wasira ametembelea miradi mitatu yenye thamani ya Tshs. 43,805,000/= na miradi hii inaundwa na vikundi vya watu kumi hadi kumi na wawili kwa kila kikundi. Katika Mradi wa kwanza Mhe. Wasira ametembelea kikundi cha akina mama wajane 12 katika Kijiji cha Kikuku ambao waliwezeshwa na Mradi wa TASAF Tshs. 11,032,500/= na kununua mashine za kusaga na kukoboa ambazo wanaziendesha kwa kusaga na kukoboa nafaka hasa mahindi, mradi ulianza Novemba 2009.
Mradi wa pili alioutembelea Mhe. Wasira ni Usindikaji wa ngozi katika Kijiji cha Kangantebe, mradi unaendeshwa na vijana kumi tu. TASAF II ilikiwezesha kikundi hiki cha vijana kumi Tshs. 7,772,500/= Novemba 2009 na vijana hawa wakaanzisha mradi wa kusindika ngozi kwa njia ya kienyeji. Mradi huu umeonyesha mafanikio makubwa kwani vijana hawa waliweza kumuonyesha Mhe. Waziri jinsi wanavyosindika ngozi mpaka kupata bidhaa zitokanazo na ngozi hizo ambazo ni bora na imara sana. Pia vijana hawa waliweza kumweleza Mhe. Waziri kuwa kwa hivi sasa wanajipatia Tshs. 120,000/= kila mmoja kwa mwezi kama faida.
Aidha Mhe. Wasira alitembelea mradi wa kuhifadhi mazingira ambao pia ulifadhiliwa na TASAF II katika Kijiji cha Rutenge. Mradi huu uligarimiwa kwa Tshs. 25,000,000/= ili kuhifadhi mazingira kwa kuanzisha kitalu cha miti kwa kuotesha miti na kuanzisha upandaji wa miti ili kuhifadhi mazingira. Pia mradi huu umefanikiwa kwa kiwango kikubwa kwani wanakikundi wa kikundi hiki wameweza kupanda miti kwa wingi katika maeneo mbalimbali yanayozunguka eneo la kijiji cha Rutenge.
Aidha pamoja na uwezeshaji wa Miradi kutoka TASAF II bado miradi hii inakabiliwa na changamoto kubwa tatu ambazo ni: vikundi vya miradi ambayo ni endelevu kutokuwa na ELIMU na ujuzi wa kutosha katika kuendesha miradi na ujasiliamali. Pili MTAJI mdogo ambao haukidhi haja ya kuendesha miradi endelevu. Na Changamoto ya tatu ni kutokuwa na MASOKO ya kuaminika kuuza bidhaa zinazozalishwa na vikundi hivi vya ujasiliamali.
Aidha katika kutatua changamoto hizo Mhe. Wasira amemwagiza Afisa Miradi wa TASAF Makao Makuu aliyeambatana nae Bw.Quintus Kassese kuviunganisha vikundi hivyo na asasi nyingine kama SIDO ili kupata Elimu ya ujasiliamali na ujuzi, pia katika maandalizi ya TASAF III awamu ya tatu wakumbuke kuandaa bajeti kwa ajili ya kuviongezea mtaji vikundi endelevu ili kupunguza mapungufu yaliyopo. Katika upande wa masoko Mhe. Wasira alimuagiza Mkurugenzi kushirikiana na Vikundi hivi kutafuta masoko Kagera na nje ya Kagera ili bidhaa zinazozalishwa zipate masoko ya kuaminika.
Mhe. Wasira ameshauri uongozi wa Mkoa wa Kagera kuhamasisha vijana kujiunga katika vikundi vidogo vidogo na kuanzisha kilimo cha bustani cha muda mfupi ili kujiajili wenyewe na kupata fedha haraka ambayo haichukui muda mrefu. “Vijana wakijiunga wachache wachache katika vikundi vidogo vidogo ni rahisi kuwezeshwa. Amani na utulivu katika taifa lenye vijana wengi ambao hawana kazi ni amani ya muda mfupi na ni hatari sana. Lazima tuhamasishe vijana kujiajili ili wajiingizie kipato wenyewe.” Alishauri Mhe. Wasira.