Je ugonjwa huu unaweza kuambukizwa kutoka kwa binadamu kwenda kwa binadamu?
Hapana. Ugonjwa huu hauenezwi kutoka binadamu mmoja kwenda kwa mwingine bali ugonjwa huu huenezwa na mbu aliyeambukizwa na virusi vya homa ya dengue anapomuuma binadamu..
Je,ugonjwa huu unatibika?
Ndio,Ugonjwa wa homa ya dengue unaweza kutibika kama mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa matibabu ya haraka.Hakuna tiba maalumu ya ugonjwa huu bali mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili zitakazoambatana na ugonjwa huu kama vile homa, kupungukiwa maji au damu vile vile hadi sasa hakuna chanjo kwa ajili ya kinga kwa binadamu.
Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya dengue
Kuangamiza mazalio ya mbu
Fukia madimbwi ya maji yaliyotuama au nyunyuzia dawa ya kuua vimelea vya mbu kwenye madimbwi hayo
Ondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile, vifuu vya nazi,makopo nk.
Fyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu
Funika mashimo ya maji taka kwa mfuniko imara
Kujikinga na kuumwa na mbu
Tumia dawa za kufukuza mbu“mosquito repellants”
Vaa nguo ndefu
Tumia vyandarua vilivyotibiwa
Weka wavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi
Hatua zinazochukuliwa na Wizara ya Afya na ustawi wa jamii
Kutoa taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa katika ofisi za Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na Zanzibar
Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika mkoa wa Dar es salaam na Zanzibar
Watumishi wa afya wa wilaya zote 3 za Dar es salaam wamepewa mafunzo ya ziada ya namna ya kutambua,kutibu na kuthibitisha ugonjwa huu
Kuanzishwa kwa vituo maalum vya ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika hospitali 3 za wilaya za Dar es salaam na hospitali ya Mnazi mmoja Zanzibar
Kuimarisha Utambuzi wa ugonjwa katika maabara ya NIMR, Dar es salaam
Wizara imeshapatiwa msaada na CDC wa vitendanishi(Primers na Probes) ili kuweza kuthibitisha ugonjwa huu
Kuimarisha Uwepo wa ugonjwa huu katika mbu
Wizara kwa kushirikiana na NIMR itafanya utafiti wa kuwepo kwa virusi vya ugonjwa huu katika mbu aina ya Aedes Aegypt
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kwani mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyekwisha kufariki. Vile vile wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu mara watakapoona mgonjwa yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.
|