UTEKELEZAJI NA MAFANIKIO
Kupunguza Vifo vya Watoto
Kiwango cha chanjo zote kwa watoto chini ya umri wa mwaka mmoja kimeongezeka kutoka asilimia 91 (mwaka 2005) hadi asilimia 93 (mwaka 2008). Katika kupunguza vifo vya watoto, halmashauri zote zinatekeleza mpango wa ”Intergrated Management of Childhood illness” ambao unahusika na kutibu magonjwa ya malaria, kichomi, kuharisha, surua, upungufu wa damu na utapiamulo. Vifo vya watoto wa umri chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 150/1000 mwaka 2000 hadi 112/1000 mwaka 2004 (Dermographic Health Survey of 2004).
Kupunguza Vifo vya akina mama vinavyotokana na Uzazi
Kiwango cha wajawazito waliojifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kimeongezeka kutoka asilimia 53.8 mwaka 2005 hadi asilimia 57 mwaka 2008. Katika kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi, halmashauri zote zinatekeleza mpango wa Huduma za dharura kwa wajawazito. Vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi vimepungua kutoka 135/100,000 mwaka 2005 hadi 118/100,000 mwaka 2008.
Kudhibiti ugonjwa wa Malaria
Kiwango cha wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano wanaotumia vyandarua viuatilifu kimeongezeka kutoka asilimia 35 mwaka 2003 hadi asilimia 68 mwaka 2008. Kiwango cha vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano kutokana na ugonjwa wa Malaria kimepungua kutoka asilimia 22.8 mwaka 2002 hadi asilimia 13 mwaka 2008. Aidha Mkoa haukupata mlipuko wa Malaria mwaka 2007, 2008 na 2009 kama ilivyokuwa inatokea miaka ya 1998 hadi 2006.
Hata hivyo kiwango cha Malaria Mkoani Kagera bado kiko juu (41% mwaka 2008).
Unyunyiziaji wa dawa ya ukoko majumbani ulifanyika katika wilaya za Bukoba Vijijini, Misenyi, Ngara, Biharamulo na Chato kwa awamu ya kwanza, Muleba awamu ya tatu na Karagwe awamu ya pili. Kwa ujumla zoezi hili lilifanikiwa kwa asilimia 93.6 Jedwali na 13 lahusika. Ni imani yetu kuwa iwapo litakuwa endelevu litasaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la ugonjwa wa Malaria.
Kudhibiti ugonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma
Vituo vya tiba vinavyotumia ”Direct Observed Treatments” kwa ugonjwa wa Kifua Kikuu vimeongezeka kutoka 15 mwaka 2001 hadi 68 mwaka 2008. Idadi ya vituo vya tiba vinavyotumia ”Multi Drug Therapy” kwa ugonjwa wa Ukoma vimeongezeka kutoka 40 mwaka 2003 hadi 75 mwaka 2008.
Kudhibiti UKIMWI
Utafiti uliofanywa na TACAIDS mwaka 2004 uligundua kuwa kasi ya maambukizo ya Virusi vya UKIMWI (HIV Prevalence) ilikuwa asilimia 3.7 ukilinganisha ya kitaifa ambayo ni asilimia 7. Mkoa uliendesha kampeni ya Taifa ya upimaji wa Virusi vya UKIMWI kwa hiari kuanzia tarehe 22 Septemba 2007 hadi 31 Mei 2008. Matokeo ni kuwa wananchi 259,021 kati ya walengwa 253,988 walipimwa sawa na asilimia 101.9 Aidha watu 10,478 kati ya watu 259,021 waliopimwa walikutwa na Virusi vya UKIMWI (HIV POSITIVE) sawa na asilimia 4
Upimaji wa hiari wa virusi vya UKIMWI unaendelea kutolewa kwa njia ya kawaida (routine) katika jumla ya vituo 130 vya huduma za ushauri nasaha na upimaji wa hiari (VCT).
Utafiti uliofanywa tena na TACAIDS mwaka 2008 uligundua kuwa kasi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI (HIV Prevalence) katika Mkoa wa Kagera ilikuwa asilimia 3.4 na ile ya kitaifa ilikuwa asilimia 5.7.
Kwa hiyo kiwango cha maambukizo katika Mkoa wa Kagera kimeshuka kutoka 3.7% (mwaka 2004) hadi 3.4% (mwaka 2008), na Kitaifa kiwango kimeshuka kutoka 7.0% (mwaka 2004) hadi 5.7% (mwaka 2008).
Sasa hivi Mkoa wa Kagera unashika nafasi ya tano kutoka chini kwa kiwango cha maambukizo. Mikoa yenye maambukizi ya chini sana ni Kilimanjaro (1.9%), Kigoma (1.8%), Arusha (1.6%), na Manyara (1.5%).
Mikoa yenye maambukizo ya juu ni Iringa (15.7%) na Dar es Salaam (9.3%).
Katika kudhibiti UKIMWI na madhara yake, Mkoa wa Kagera umefanikiwa kufungua vituo vya huduma (Care and Treatment) 44, na vituo 168 vinavyotoa huduma ya kuzuia maambukizo kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto (PMTCT).
Kuanzia Mei 2005 hadi Juni 2009 jumla ya wateja waliandikishwa na kuhudumiwa katika vituo vya CTC.
Maboresho katika Sekta ya Afya
Lengo la mabadiliko yanayofanyika katika Sekta ya afya ni kuboresha huduma na kusambaza huduma za afya katika maeneo ya vijijini ambapo asilimia 80 ya wananchi wanaishi. Katika kutoa madaraka zaidi kwa halmashauri juu ya uendeshaji wa huduma za afya, Bodi za afya (Council Health Service Boards) na kamati za vituo vya afya na Zahanati zilianzishwa na kuimarishwa. Mpango wa ”Indent System” umeanzishwa katika halmashauri zote ili kuhakikisha kwamba dawa na vifaa muhimu vinapatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya. Katika kutafuta vyanzo vipya vya fedha za kuendeshea huduma za afya Halmashauri ya Karagwe imeanzisha mfuko wa afya ya Jamii (Community Health Fund). Aidha halmashauri zingine ziko kwenye hatua mbali mbali za kuanzisha mfuko huo wa afya ya jamii. CHANGAMOTO
Mkoa unakabiliwa na matatizo yanayoathiri utoaji bora afya.
Mkoa una upungufu wa watumishi wenye stadi na ujuzi unaotakiwa
Mkoa bado una upungufu wa zahanati 442 Vituo vya afya 125 na hospitali 6.
Mkoa una upungufu wa vitendea kazi.
MIKAKATI
Sera ya Taifa ya afya ni kusogeza huduma za afya karibu na wananchi. Kwa hiyo matarajio ya Mkoa ni kutekeleza mpango wa maendeleo ya afya (MMAM).
Katika kutekeleza sera hiyo mkoa umeandaa mpango wa ujenzi wa zahanati katika kila kijiji na Kituo cha afya katika kila kata.
Ujenzi rasmi wa zahanati na vituo vya afya vipya umeanza mwaka huu wa fedha 2008/2009.
Mkoa wa Kagera utaendesha Kampeni ya ugawaji wa vyandarua bila malipo kwa watoto chini ya miaka mitano, uwekaji wa dawa ya ngao iliyoboreshwa kwenye vyandarua vilivyo majumbani, na upuliziaji dawa ya ukoko majumbani kila mwaka mara moja
Katika kutafuta vyanzo vipya vya fedha za kuendesha huduma za afya, halmashauri zote za Mkoa wa Kagera kasoro Karagwe, zinashauriwa kuanzisha mfuko wa afya ya jamii (Community Health Fund).
|