JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OFISI YA MKUU WA MKOA KAGERA
     
 
     
 
 
     
TAARIFA YA HIFADHI YA MAZINGIRA - MKOA WA KAGERA
[ Nyumbani ] au
 
UTANGULIZI
 

Mkoa wa Kagera umeendelea kutekeleza Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997 kwa kuandaa na kutekeleza mikakati iliyowekwa. Katika kutekeleza mikakati hiyo, Mkoa umeendelea kuhamasisha wananchi kuhifadhi Mazingira kwa njia mabalimbali ikiwemo kutoa elimu ya mazingira. Halmashauri za wilaya na Manispaa mkoani Kagera zimeshiriki katika mashindano ya kitaifa ya usafi chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Aidha, wananchi na Taasisi mbalimbali zimeshiriki katika mashindano ya Tuzo ya Rais ya Kuhifadhi mazingira ya ardhi kupanda na kutunza miti ambapo washindi kimkoa wamepatikana, hivi sasa mchakato wa kitaifa unaendelea. Juhudi nyingine zinazofanywa ni kufanya doria za mara kwa mara ili kudhibiti ufugaji, uvuvi na uvunaji misitu usio endelevu.

Athari kubwa za uharibifu wa mazingira zinazoukabili mkoa wa Kagera ni pamoja na uchungaji holela wa mifugo, ukataji miti na uchomaji moto ovyo misitu, uvuvi haramu, ujenzi holela katika miji na kando kando ya vyanzo vya maji, uthibiti dhaifu wa maji machafu na taka ngumu, pamoja na kilimo katika vyanzo vya maji na miteremko.

 

 

 

 
 
 
 

UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA HIFADHI NA UENDELEZAJI WA MISITU

 

Katika kipindi cha 2009/2010 Mkoa ulijiwekea Mkakati wa kutoa Elimu kwa Wananchi ili kukuza Weledi wao kuhusu dhana ya uhifadhi wa Mazingira pamoja na viambata vyake. Elimu ilitolewa kwa njia ya Mikutano, Warsha na Semina kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Maendeleo kama vile World Vision, SCC –Vi Agro forestry, KADETF, ECOVIC, KIROYERA TOURS, REDESO, TADEPA na CHEMA.

Halmashauri za Wilaya pamoja na Manispaa Mkoani Kagera zimesimamia kampeini za upandaji miti na utoaji wa elimu ya hifadhi ya Mazingira kwa wananchi.

 

 

 
 
 
UPANDAJI NA UTUNZAJI WA MITI
 

Shughuli ya upandaji wa ukuzaji wa Miti imetekelezwa na kila Wilaya kwa kuzingatia malengo na Mikakati waliyojiwekea pamoja na agizo la Serikali la kupanda Miti 1,500,000 kila Wilaya kwa mwaka. Mchanganuo wa malengo na Miti iliyopandwa katika kila Wilaya unaojionesha katika Jedwali hapa chini.

WILAYA

LENGO

(Miti)

UTEKELEZAJI

2008/09

IDADI YA MITI ILIYOPONA

BIHARAMULO

1,500,000

1,200,000

1,127,400

BUKOBA (V)

1,500,000

1,382,940

1,275,500

KARAGWE

1,500,000

1,506,847

1,442,760

MANISPAA

500,000

415,000

402,115

CHATO

1,500,000

1,265,400

1,250,000

MISSENYI

1,500,000

1,416,500

1,366,310

MULEBA

1,500,000

1,307,450

1,218,400

NGARA

1,500,000

1,859,160

1,805,550

 

11,000,000

10,353,927

9,888,035

 

 

 
Matumizi ya majiko sanifu na Nishati Mbadala
 

Wilaya kwa kushirikiana na Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO's) wanaendelea kuhamasisha Wananchi kuhusu Matumizi ya Nishati mbadala kama vile jua,gesi na majiko yanayotumia kuni/Mkaa kidogo(Majiko banifu). Lengo la Serikali ni kupunguza zaidi matumizi ya Mkaa ambao ni moja kati ya vyanzo vikubwa vya uharibifu wa mazingira.

Katika utekelezaji wa Mkakati huu, kwa kipindi kinachoishia Novemba, 2009 jumla ya wananchi 248 wamepata mafunzo ya teknolojia ya utengenezaji wa majiko sanifu na matumizi ya Nishati mbadala katika Wilaya za Chato, Ngara, Muleba, Biharamulo na Karagwe. Kama inavyonesha kwenye Jedwali. Idadi ya majiko sanifu yaliyotengenezwa katika kipindi hiki ni 48760. Uhamasishaji bado unaendelea kwa kutumia vikundi vya jamii vya Hifadhi ya Mazingira katika Kata na Vijiji.

 

 

Changamoto za hifadhi ya mazingira

Pamoja na mafanikio na hatua kubwa tuliyopiga katika kutekeleza Sera na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na.20 ya mwaka 2004, bado tunakabiliwa na changamoto nyingi ili kufikia malengo makuu ya program zetu za Hifadhi ya Mazingira. Changamoto zinazotukabili ni:-

•  Uchomaji moto ovyo (mioto kichaa) unaendelea kufanyika katika Wilaya zote za Mkoa wetu

•  Ukataji holela wa miti katika Misitu ya Hifadhi kwa ajili ya uchomaji Mkaaa na upasuaji haramu wa Mbao.

•  Kukauka kwa vyanzo vya maji kutokana na uchomaji misitu, ukataji holela wa miti na Kilimo kandokando ya mito na vyanzo vya maji.

•  Kuvamiwa Misitu ya Hifadhi na Mapori ya Akiba kwa ajili ya uchungaji wa mifugo, uchimbaji madini na Kilimo kisicho endelevu.

•  Ufinyu wa Bajeti kwa ajili ya shughuli za Uendelezaji na usimamizi wa Rasilimali za misitu na Hifadhi ya mazingira.

•  Kufanyika kwa uvuvi usioendelevu wa kutumia zana haramu kama mabomu, sumu, makokoro na nyavu zenye macho madogo chini ya Inchi 5.

•  Urinaji asali usio endelevu hasa kwa kutumia moto.

•  Utupaji ovyo wa taka ngumu katika maeneo ya miji, vitongoji na vijiji vyetu.

Katika kukabiliana na changamoto hizi, Mkoa umeamua kuanza kutekeleza zoezi la utoaji wa Tuzo ya Mheshimiwa Rais ya Kuhifadhi vyanzo vya Maji, Kupanda na Kutunza miti. Kwa kuanzia Mkoa uliendesha semina ya maelekezo kwa Maafisa Ardhi, Maliasili na Mazingira wa Wilaya zote za Mkoa wa Kagera mnamo mwezi Septemba mwaka 2009. Mwongozo ulitolewa kwa Maafisa hawa waandamizi ili wakawawezeshe na kuwahamasisha Wananchi kushiriki katika mashindano ya Tuzo ya Rais ya Kuhifadhi Mazingira.

 

“Inawezekana kila mmoja akitekeleza wajibu wake.

 

 
 

 

 

 

 

 

 
 
 
 
 
 
 
Udhibiti wa gugu maji katika ziwa na mito
 

Shughuli ya udhibiti wa gugu maji katika ziwa Victoria pamoja na mito/mabwawa iliendelea kufanyika kwa kutumia njia husishi (Biological control). Katika njia hii husishi wadudu aina ya MBAWA KAVU (Water Hyacirth weevils) ndiyo hutumika kuangamiza gugu maji. Wadudu hawa ni Rafiki wa mazingira kwani hawana madhara yoyote kwa viumbe wengine.

Utafiti unaendelea kufanyika kuhusu njia ya kudhibiti gugu maji ndani ya mto Kagera na mito mingine maana mdudu wa MBAWA KAVU hawezi kufanya kazi yake vizuri kwenye mito kutokana na kasi ya maji. Wataalamu wanaangalia uwezekano wa kutumia mdudu mbadala aina ya MITES.

Hifadhi ya Mazingira ya Miji na Utupaji Taka

Katika kuadhimisha siku ya mazingira Duniani mwaka huu, kila Wilaya ilielekezwa kuandaa Program ya maadhimisho haya. Mingoni mwa shughuli zilizoainishwa katika program za Wilaya zote ni kusafisha mitaro, kufanya usafi katika maeneo ya makazi, maeneo ya biashara (Masoko) pamoja na kuhimiza utumiaji wa mashimo au vyombo vya kutupia taka za majumbani.

Utekelezaji wa program hizi za Wilaya bado ni hafifu isipokuwa kwa Wilaya ya Karagwe ambao wametekeleza Program yao kwa zaidi ya asilimia 90.

Ziara ya ujumbe wa Ofisi ya Makamu wa Rais

Katika kipindi hiki kuanzia tarehe 26 Julai hadi 30 Julai, 2009 Mkoa ulitembelewa na ujumbe kutoka ofisi ya Makamu wa Rais kwa ajili ya kukagua na kuona hali halisi ya mazingira. Ujumbe wa Ofisi ya Makamu wa Rais uliongozwa na Katibu Mkuu (OMR) Bibi Ruth Mollel. Ujumbe uliweza kutembelea na kukagua shughuli za Hifadhi ya mazingira katika Wilaya za Bukoba Vijijini, Muleba, Missenyi na Manispaa ya Bukoba.

Baada ya ziara hiyo ya siku nne, Ofisi ya Makamu wa Rais iliuandikia Mkoa barua ya Pongezi kutokana na jitihada zinazofanywa na viongozi pamoja na Wananchi katika kuhifadhi Mazingira. Aidha, Mkoa umeelekezwa kuendelea kuhamasisha jamii katika upandaji wa miti pamoja na kuepuka uchomaji moto ovyo.

Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi

Kauli Mbiu ya maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani Mwaka 2009 ilikuwa ni “ Dunia inakuhitaji; Tuungane kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi”. Muhtadhari wa kauli Mbiu hii ni kuhimiza uwajibikaji wa kila mtu na kila sekta katika Kupambana na kujiweka tayari kukabiliana na mabadiliko ya Tabia nchi kwa kuhifadhi mazingira.

Chanzo kikuu cha mabadiliko ya Tabianchi (climate change) ni kuongezeka kwa joto Duniani. Kuongezeka kwa joto kunasabishwa na gesijoto ( green - house gases ) kwa kiwango kikubwa kuliko kiasi halisi kinachohitajika kuwezesha uhai na mifumo ya Dunia kuwa katika hali yake ya asili. Katika mazingira yetu, gesijoto ni Carbon-Dioxide, Methani na nyinginezo ambazo zinatokana na shughuli za kila siku za Mwanadamu, kwa mfano viwanda, vyombo vya usafirishaji, ukataji misitu, uchomaji moto ovyo pamoja na kilimo kisicho endelevu.

Athari za mabadiliko ya Tabianchi zinazoweza kutukabili tusipochukua tahadhari ni:-

•  Kubadilika na kutotabirika kwa misimu ya mvua.

•  Kushuka au kupungua kwa mavuno katika mashamba.

•  Kuongezeka kwa majanga ya mafuriko/ukame

•  Kupungua kwa theluji katika vilele vya milima (mfano mlima Kilimanjaro) kwa kasi kubwa.

•  Kushuka au kupungua kwa kina cha maji katika mito na maziwa.

•  Kuenea kwa maradhi ya Malaria hata kwenye maeneo yenye baridi ya hali ya juu kama vile Bukoba, Ngara na Karagwe

Ili kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, sote kwa pamoja tunasisitizwa kuendelea kuchukua hatua za dhati, kwa kutumia nyadhifa zetu, kuzuia uharibifu wa mazingira na kuboresha palipo haribika. Tayari Serikali imetuandalia “ Silaha ” tatu za kupambana na adui yetu huyu, nazo si nyingine bali ni:-

•  Sheria ya Usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004

•  Mpango wa Taifa wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (2006)

•  Mkakati wa Taifa wa Kuhifadhi Mazingira ya Ardhi na vyanzo vya Maji (2006).

 

 

 
 
 
 

 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 
[ Nyumbani ] au
Rudi juu
 
     
Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa KAGERA, BUKOBA, TEL: 028 - 2220215/17, FAX: 028-2752184