JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OFISI YA MKUU WA MKOA KAGERA
     
 
     
 
 
     

 

 
[ Nyumbani ] au
 

TAARIFA YA MAENDELEO YA KILIMO MKOANI KAGERA MSIMU WA KILIMO 2009/2010

HALI YA HEWA

 

Katika msimu wa Vuli 2008/09 takwimu za mvua zilizopatikana kutoka kituo cha Uwanja wa Ndege Bukoba zinaonesha kuwa mvua zilikuwa haba (727.8 mm kwa siku 65) ukilinganisha na mvua za vuli za miaka miwili ya nyuma (997.2 mm kwa siku 82 mwaka 2006 na 897.0 mm kwa siku 67 mwaka 2007). Hivyo wakulima ama walichelewa sana kupanda mazao yao au mazao yaliyopandwa mwezi Septemba 2008 yalikabiliwa na ukame.

Upatikanaji mvua tangu msimu wa kilimo 2009/2010 uanze umekuwa siyo wa kuridhisha katika maeneo mengi ya Mkoa wa Kagera; ijapokuwa Taasisi ya Hali ya Hewa Tanzania ilitabiri kwamba mvua za msimu wa Vuli 2009 katika Kanda ya Ziwa zitanyesha kwa kiwango cha juu ya wastani na kusababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo ya mabonde. Hadi mwishoni mwa Septemba 2009 baadhi ya maeneo katika wilaya zote yalikuwa hayajapata mvua za uhakika, na hivyo wakulima ama wamechelewa sana kupanda mazao yao au mazao yaliyopandwa mwezi Septemba 2009 yalikabiliwa na ukame

 

 

 
 
 

UTEKELEZAJI WA MPANGO WA KILIMO MSIMU 2008/2009 .

Utekelezaji wa Malengo ya Kilimo Msimu 2008/2009

Katika msimu wa kilimo 2008/2009 Mkoa ulijiwekea lengo la kulima na kutunza jumla ya hekta 828,700 za mazao mbalimbali ya chakula zilizotarajiwa kuzalisha jumla ya tani 1,270,210 za ndizi, tani 399,670 za nafaka, tani 95,670 za mikunde na tani 1,526,625 za mazao ya mizizi.

Aidha, mkoa ulilenga kulima na kutunza jumla ya hekta 171,400 za mazao mbalimbali ya biashara zilizotarajiwa kuzalisha jumla ya tani 57,310 za kahawa, tani 198 za tumbaku, tani 9,940 za pamba mbegu, tani 4,170 za majani mabichi ya Chai.

Hadi tarehe 30 Juni 2009 inakadiriwa kwamba Mkoa ulikuwa umelima na kutunza jumla ya hekta 662,200 za mazao mbalimbali ya chakula na kuzalisha jumla ya tani 1,175,500 za ndizi, tani 242,200 za nafaka mbalimbali, tani 136,200 za mikunde na tani 629,900 za mazao mbalimbali ya mizizi.

Aidha, hadi tarehe 30 Juni 2009 inakadiriwa kwamba Mkoa ulikuwa umelima na kutunza jumla ya hekta 110,100 za mazao mbalimbali ya biashara na kuzalisha jumla ya tani 55,000 za Kahawa maganda , tani 6,500 za Pamba mbegu, tani 150 za Tumbaku na tani 3,300 za Majani mabichi ya Chai

Upatikanaji wa Chakula Hadi Juni 2009

Mahitaji ya chakula mwaka 2009 kwa wakazi wa mkoa wa Kagera yalikuwa tani za metriki 585,980 za wanga na tani za metriki 58,598 za mikunde.

Tathmini ya awali ya hali ya uzalishaji wa mazao msimu 2008/2009 na matarajio ya upatikanaji chakula msimu 2009/2010 ilifanyika katika Wilaya zote mkoani Kagera tarehe 18-24 Mei, 2009, kwa kushirikiana na wataalam kutoka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Ofisi ya Waziri Mkuu na World Food Programme (WFP). Tathmini hiyo ilieonesha kuwa wilaya zote mkoani Kagera zilikuwa na chakula cha kutosha, na hali ya upatikanaji msimu wa 2009/2010 ilitabiriwa kuwa ya kuridhisha.

Hadi 30 Juni 2009 Wilaya zote zinazostawisha zao la ndizi na muhogo ziliripoti kwamba mazao hayo yalikuwa yanapatikana kwa kiwango kikubwa na ziada ilikuwa inauzwa nje ya mkoa; na mahali penginepo vyakula vingine vingi vilikuwa vinapatikana kwa kiwango cha kuridhisha.

  Ununuzi wa Mazao ya Biashara Hadi Juni 2009

Kahawa Maganda

Msimu wa ununuzi 2008/2009 bei za Buni (Kahawa m aganda ) kwa wanunuzi walio wengi zilianzia kwenye wastani wa TShs 750/= kwa kilogramu; lakini mwishoni mwa msimu wa ununuzi ziliteremka kufikia wastani wa TShs 350/=, kwa sababu za kuanguka kwa bei katika soko la dunia.

Hadi 30 Juni 2009 jumla ya tani 52,457 za Buni (Kahawa maganda) zenye thamani ya Tshs. 39,342,624,750/= zilikuwa zimenunuliwa mkoani kote.

Pamba Mbegu

Makampuni sita ya binafsi yalinunua pamba wilayani Biharamulo na Chato, na bei ya wastani ilikuwa ni TSh 400/= kwa kilogramu. Hadi mwisho wa msimu wa ununuzi 2008/2009 tani 6,500 za Pamba mbegu zenye thamani ya TSh 2,600,000,000/= zilinunuliwa.

Majani Chai

Majani ya chai hulimwa katika wilaya za Bukoba na Muleba na Msimu wake anza mwezi Septemba. Zao hili hununuliwa na Maruku Tea Estate Company Ltd. Bei ya majani mabichi ya chai ilikuwa TShs 100/= kwa kilogramu na kufikia 30 Juni 2009 Kilogramu 2,868,159 za Majani ya Chai mabichi zenye thamani ya TShs 286,815,900/= zilinunuliwa.

Tumbaku Tumbaku hulimwa katika wilaya ya Biharamulo na Chato, na msimu wake wa ununuzi huanza mwezi Aprili. Ununuzi wa zao hilo ulioanza mwezi Aprili 2009 ulifanywa na Tanzania Leaf Tobacco Company (TLTC). Hadi 30 Juni 2009 tani 186 za tumbaku zilinunuliwa zenye thamani ya TShs 491,040,000/=.

 

 

 
 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 

 

 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 
 
 
MPANGO WA KILIMO MSIMU 2009/2010
 

Malengo ya Kilimo Msimu 2009/2010

Katika msimu wa kilimo 2009/2010 Mkoa umejiwekea lengo la kulima na kutunza jumla ya hekta 738,300 za mazao mbalimbali ya chakula zilizotarajiwa kuzalisha jumla ya tani 1,369,800 za ndizi, tani 355,700 za nafaka, tani 130,300 za mikunde na tani 995,600 za mazao ya mizizi.

Aidha, mkoa umelenga kulima na kutunza jumla ya hekta 105,000 za mazao mbalimbali ya biashara zilizotarajiwa kuzalisha jumla ya tani 40,000 za kahawa, tani 220 za tumbaku, tani 16,000 za pamba mbegu, tani 4,500 za majani mabichi ya Chai.

Mahitaji na Upatikanaji wa Chakula Msimu 2009/2010

Inakadiriwa kuwa mwaka 2010 idadi ya wakazi wa mkoa wa Kagera itafikia 2,563,800 (maoteo). Mahitaji ya chakula kwa wakazi wa mkoa huu kwa mwaka 2010 ni tani za metriki 608,260 za wanga na tani za metriki 60,820 za mikunde. Hadi mwisho wa Septemba 2009 wilaya zote ziliripoti kwamba katika maeneo mengi chakula kilikuwa kinapatikana kwa kiwango cha wastani, japokuwa kuna maeneo machache ambayo yalikuwa na upungufu.

Inatarajiwa kwamba katika msimu wa kilimo 2009/2010 mkoa wa Kagera utaweza kujitosheleza kwa chakula, japokuwa ziada kwa ajili ya kuuza itakuwa ndogo. Hali ya upungufu mkubwa wa chakula inaweza kujitokeza katika maeneo kadha kama mvua za Vuli hazitaendelea hadi mwisho wa Desemba 2009

Malengo ya Ununuzi wa Mazao Msimu 2009/2010

Kahawa Maganda

Katika msimu wa ununuzi 2009/2010 makisio ya ununuzi wa kahawa kwa mkoa mzima wa Kagera ni tani 34,015 kwa wastani wa TSh 450/= kwa Kilogramu. Kiasi hiki ni kidogo ukilinganisha na msimu wa ununuzi 2008/2009, kwa sababu mvua zilinyesha mfululizo katika kipindi cha kutunga maua na hivyo maua mengi yalioza. Hadi 15 Oktoba Kilogramu 19,005,270 zenye thamani ya TShs 8,552,371,500.00 zilikwishanunuliwa.

Pamba Mbegu

Katika msimu wa 2009/2010 makisio ya ununuzi wa pamba mbegu ni tani11,800, kwa bei ya sasa ya TSh 440/= kwa kilogramu. Hadi 15 Oktoba 2009, Kilogramu 4,092,730 zenye thamani ya TShs 1,800,801,200.00 zilikwishanunuliwa.

Majani Chai

Katika msimu wa 2009/2010 makisio ya ununuzi ni tani 3,500 kwa bei ya sasa ya TSh 110/= kwa kilogramu. Msimu mpya wa ununuzi wa majani chai umeanza 01 Oktoba 2009.

Tumbaku

Katika msimu wa 2009/2010 makisio ya ununuzi ni tani 200 kwa bei ya sasa ya TSh 2,640/= kwa kilogramu. Msimu wa ununuzi wa tumbaku utaanza Aprili 2010.

MPANGO WA HALMASHAURI WA KUNUNUA MATREKTA YA MKONO (Power Tillers).

Agizo la Waziri Mkuu kuhusu kila Halmashauri ya Wilaya kujiwekea utaratibu wa kununua Power Tillers 50 na Power Tillers 20 kwa kila Manispaa kila mwaka, ulipokelewa wakati Halmashauri zimekwishakamilisha utaratibu wa kuandaa na kupitisha bajeti kwenye vikao vyote halali vya Hamashauri, na kuwasilisha bajeti hizo katika ngazi za juu kwa kuzingatia Ukomo wa Bajeti. Agizo hilo litaendelea kutekelezwa katika bajeti zijazo kama alivyoagiza Waziri Mkuu.

Katika bajeti ya mwaka 2009/2010 Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Kagera zimepanga kununua jumla ya matrekta ya mkono (Power Tillers) 97 kupitia Mipango ya Kuendeleza Kilimo Wilayani (DADPs), kwa gharama ya TShs 824,337,700 /= kwa mchanganuo ufuatao:

•  H/Wilaya Biharamulo – Matrekta ya Mkono 13 kwa gharama ya TSh 84,000,000.00

•  H/Wilaya Muleba – Matrekta ya Mkono 5 kwa gharama ya TSh 34,500,000.00

•  H/Wilaya Bukoba – Matrekta ya Mkono 15 kwa gharama ya TSh 120,000,000.00

•  H/Wilaya Karagwe – Matrekta ya Mkono 8 kwa gharama ya TSh 77,837,700.00

•  H/Manispaa Bukoba – Matrekta ya Mkono 0 kwa gharama ya TSh 0.00

•  H/Wilaya Chato – Matrekta ya Mkono 20 kwa gharama ya TSh 160,000,000.00

•  H/Wilaya Missenyi – Matrekta ya Mkono 6 kwa gharama ya TSh 48,000,000.00

•  H/Wilaya Ngara – Matrekta ya Mkono 30 kwa gharama ya TSh 300,000,000.00

MAAGIZO MAALUM YA SERIKALI KUHUSU KILIMO KWANZA

Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lilifanya mkutano tarehe 2 na 3 mwezi Juni 2009 jijini Dar es Salaam, kujadili sera na mikakati ya kuleta mapinduzi ya kilimo cha Tanzania pamoja na utekelezaji wake chini ya kaulimbiu ya “ KILIMO KWANZA

Kwa kutambua kuwa changamoto kubwa kwa Tanzania ni kupambana na umaskini na kwamba hili litawezekana hasa kwa kuongeza tija katika kilimo, mkutano huo uliazimia na kuagiza yafuatayo:

•  KILIMO KWANZA iwe ndiyo dhana ya kuleta mapinduzi ya kijani kwa lengo la kukifanya kilimo cha Tanzania kuwa cha kisasa na cha kibiashara;

•  Dhana ya KILIMO KWANZA ijumuishwe kwenye mipango mbalimbali ya Serikali ili kuhakikisha mafanikio ya utekelezaji wake;

•  Jitihada zifanyike katika kuongeza rasilimali mbalimbali ili kufanikisha utekelezaji wa KILIMO KWANZA ;

•  Sekta binafsi ihamasishwe ili iongeze uwekezaji kulingana na wajibu wake katika utekelezaji wa KILIMO KWANZA ; na

•  Utekelezaji wa KILIMO KWANZA utaongozwa na nguzo kumi zifuatazo:

• I. Utashi wa kisiasa kutoa msukumo wa mapinduzi ya Kilimo.

• II. Kugharamia mapinduzi ya Kilimo

• III. Uboreshaji wa mfumo wa utawala wa kilimo.

• IV. Mabadiliko ya mfumo mkakati katika kilimo.

• V. Upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya kilimo.

• VI. Vivutio vya kuchochea uwekezaji katika kilimo.

• VII. Uendelezaji wa viwanda katika kuleta mapinduzi ya kilimo.

• VIII. Sayansi, Teknolojia na Rasilimali Watu katika kuwezesha mapinduzi ya kilimo.

• IX. Uendelezaji wa Miundombinu ili kuwezesha mapinduzi ya kilimo.

• X. Uhamasishaji na ushirikishwaji wa Watanzania kuunga mkono na kutekeleza KILIMO KWANZA .

Maelezo kamilifu ya nguzo hizi kumi yaliyofafanuliwa katika programu ya kitaifa yamekwishatolewa. Mkoa umetekeleza hatua ya kwanza ya programu za Kitaifa kwa kuitisha mkutano wa wadau tarehe 22-23 Desemba, 2009, ambao ulipitia na kujadili nguzo zote za KILIMO KWANZA na hatimaye kuweka mikakati na mbinu za utekelezaji wa kila jukumu la kutekeleza shughuli za KILIMO KWANZA.

Baada ya mkutano huo, kila Wilaya/Halmashauri ilielekezwa kupitia upya maazimio ya mkutano na kutengeneza upya mpangomkakati wa kutekeleza KILIMO KWANZA unaoonesha vipaumbele vya Wilaya na viashiria vya kupima utekelezaji wa kila mkakati.

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 
[ Nyumbani ] au
Rudi juu
 
     
Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa KAGERA, BUKOBA, TEL: 028 - 2220215/17, FAX: 028-2752184