Mkuu wa Mkoa Mstaafu Mhe. Babu ameitumikia serikali kwa miaka ipatayo 40 katika utumishi wa umma. Mhe. Babu anasema baada ya kumaliza Elimu ya Juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1971 alianza kazi kama Afisa Mipango wa Wilaya katika utumishi wa umma.
Historia ya Mhe. Babu ni ya kipekee kwani amepitia ngazi mbalimbali za kiutendaji na uongozi kuanzia ngazi ya Halmashauri mpaka Mkoa. Alianza kazi akiwa kama Afisa Mipango wa Wilaya, alipanda cheo na kuwa Mkurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya (Mkurugenzi wa Halmashauri), Mhe. Babu Alipanda tena cheo na kuwa Mkurugenzi wa Maendeleo wa Mkoa (R.D.D) wakati huo, kwa sasa (Katibu Tawala Mkoa).
Mwaka 1996 Mhe. Babu aliteuliwa rasmi na Mhe. Benjamini Mkapa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo kuwa Mkuu wa Mkoa. Mhe. Babu alianza kazi yake kama Mkuu wa Mkoa wa Kagera kuanzia mwaka 1996 akiwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera wa 16, baadae alihamishwa kituo cha kazi mwaka 1999 kwenda Shinyanga kwa wadhifa huo huo, kisha Mkoa wa Arusha na baadaye Kilimanjaro. Aidha mwaka 2009 Mhe. Babu alirudishwa Mkoa wa Kagera tena na kuwa Mkuu wa Mkoa wa 19 mpaka anastaafu Septemba 14, 2011.
Mkuu wa Mkoa Mstaafu Mhe. M. A. Babu amewahusia watumishi wote wa umma hususani Mkoa wa Kagera mambo makuu mawili ya kuzingatia sana katika utumishi wa umma, la kwanza ni kila mtumishi wa umma kufanya kazi zake kwa kuzingatia kanuni na sheria za kazi zake. Suala la pili ni watumishi wa umma kujiendeleza kielimu kuendana na hali halisi ya ushindani wa kielimu ili kufanikisha utendaji mzuri katika kutekeleza majukumu ya utumishi wa umma.
Mkuu wa Mkoa Mstaafu Mhe. Mohammed A. Babu alianzia kazi ya Ukuu wa Mkoa wa Kagera na amestaafu akiwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwa mujibu wa sheria na mashariti ya cheo cha Ukuu wa Mkoa. |