JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OFISI YA MKUU WA MKOA KAGERA
     
 
     
 
 
     
 
Habari mpya [ Nyumbani ] au
 

TAARIFA YA BODI YA BARABARA YA MKOA

 

Kikao cha Bodi ya Barabara kimefanyika Mkoani Kagera na kubainisha changamoto mbalimbali zinazoikabili miundombinu ya barabara katika Mkoa wa Kagera pamoja na utatuzi wake. Aidha pamoja na changamoto zilizopo lakini barabara za Mkoa na Halmashauri za Wilaya Mkoa wa Kagera zinaridhisha na zinapitika kwa muda wote.

Kikao hicho kilifanyika tarehe 12/03/2011 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera na kuongozwa na Mhe. Mohammed A. Babu Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Mwenyekiti wa kikao hicho. Mhe. Babu katika ufunguzi aliwapongeza wajumbe wa kikao kwa kuendelea kutunza barabara zote za Mkoa wa Kagera na kupitika kwa kipindi chote kwa mwaka mzima .

Pia Mhe. Babu aliwajulisha wajumbe wapya wa kikao hicho ambao ni Waheshimiwa Wabunge kuwa Bodi ya Barabara ya Mkoa si Bodi ya Utendaji yaani “Executive Board” bali ni Bodi ya Ushauri ambayo majukumu makubwa ni kujadili na kutoa ushauri kwa Waziri wa Ujenzi ambaye ndiye mwenye dhamana ya ujenzi, matengenezo na utunzaji wa barabara na madaraja ili kuleta tija na thamani halisi ya fedha inayotolewa na jinsi inavyotumika.

Changamoto ambayo imejitokeza kuanzia mwishoni mwa mwaka jana 2010 ni kusuasua na kupelekea kusimama kwa miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya Kagoma – Lusahunga (km 154); Ushirombo – Lusahunga (km 110) na Kyaka – Bugene (km 59) kutokana na madeni ya malipo ya kazi ambazo tayari zimekwisha kukaguliwa na kuthaminiwa. Pamoja na changamoto hiyo Mhe. Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwahakikishia wananchi wa Mkoa wa Kagera alipokuwa anafanya majumuisho ya ziara yake Mkoani Kagera kuwa fedha tayari zimelipwa na ujenzi wa barabara utaendelea mara moja.

Pia barabara zilizopandishwa hadhi/daraja ambazo ni Kyaka – Bugene – Kasulo (km 178); Omugakorongo – Kigarama – Murongo (km 106); Rutenge – Rubale – Izimbya – Omubweya – Buhamila – kishoju – (km 71) pia na Mukungo – Nyabusozi – Kabunda – Nyantakara (km 85.23) zimeendelea kupata matengenezo ya aina mbalimbali tangu zianze kuhudumiwa na Wakala wa Barabara. “Serikali inaendelea kutafuta vyanzo vingine vya fedha badala ya kutegemea mfuko wa barabara (Road Fund) pekee kama ilivyo sasa ili barabara zote zijengwe.” Alisema Mhe. Babu.

 

 

 

 
 
 
 

 

 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 

 

 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 
 
 

 

Aidha wajumbe walibainisha changamoto nyingine zinazoikabili miundombinu ya barabara Mkoani Kagera kuwa ni kutokuwepo kwa alama za barabarani wakati wa matengenezo ya kukarabati barabara, kuiba nguzo za alama za barabara na makalvati kwa ajili ya vyuma chakavu, na kumwaga mafuta barabarani ambapo mambo haya yote yanaleta uharibifu mkubwa kwenye barabara.

Kwa upande mwingine Meneja wa Wakala wa Barabara wa Mkoa (TANROADS) alibainisha changamoto kubwa ni kutokuwepo na makampuni ya kukodisha mitambo ya ujenzi wa barabara kwa Makandalasi waliopo jambo ambalo linapelekea shughuli nyingi za ujenzi wa barabara kukwama. Pia magari makubwa kuzidisha uzito na kuharibu barabara.

Katika utatuzi wa changamoto hizo Mhe. Babu aliwaomba wajumbe kushirikiana kwa pamoja kulinda miundombinu ya barabara na kuitunza pia na kushirikiana na Wakala wa Barabara wa Mkoa (TANROADS) na sio kuzichukulia baadhi ya barabara kuwa ni za Halmashauri au Mkoa kwa sababu serikali ni moja na fedha za kuhudumia barabara hizo zote zinatoka kwenye serikali moja.

 

 

 
 
 

 

 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 
Habari mpya [ Nyumbani ] au
Rudi juu
 
     
Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa KAGERA, BUKOBA, TEL: 028 - 2220215/17, FAX: 028-2752184