JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OFISI YA MKUU WA MKOA KAGERA
     
 
     
 
 
     
 
 
[ Nyumbani ] au
 

BARAZA LA WAFANYAKAZI SEKRETARIETI YA MKOA WA KAGERA LAZINDULIWA RASMI NA MKUU WA MKOA

 

 

Baraza la Wafanyakazi Sekretarieti ya Mkoa wa Kagera limezinduliwa rasmi tarehe 27/05/2011na Mhe. Mohammed A. Babu katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa Kagera. Katika uzinduzi huo Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Kagera alitoa nasaha zake kwa Baraza hilo lenye wajumbe wapya na zifuatazo ni nasaha zake alizozitoa katika hotuba yake;

Nawapongeza sana kwa kufanya uchaguzi uliofanyika tarehe 22 – 26 Machi 2010 ambapo wajumbe wapya 62 walichaguliwa kulingana na mkataba mpya wa Baraza la Wafanyakazi Mkoa wa Kagera.

Idadi hii ya wajumbe inafanya maeneo yote ya Sekretarieti kuwa na wawakilishi kwenye Baraza hili.

Kwa hiyo, kwa namna ya pekee napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza wajumbe wote kwa kuchaguliwa kwenu kuwa viongozi na wajumbe wa Baraza hili. Kuchaguliwa kwenu kunatokana na uwezo mlionao katika kutekeleza majukumu yenu kama wajumbe wa Baraza hili muhimu. Aidha ni matumaini yangu kuwa mtatumia dhamana hiyo kuimarisha mahusiano baina ya mwajiri na watumishi wenzenu wa Sekretarieti ya Mkoa wa Kagera. Mahusiano baina ya mwajiri wenu na watumishi wenzenu yanategemea jinsi mtakavyotekeleza wajibu wenu kama ilivyoainishwa kwenye sheria.

Kwa kupitia Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma (Public Service Negotiating Machinery Act) Na. 19 ya mwaka 2003, Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kuwashirikisha watumishi wa Umma katika hatua mbalimbali za kutoa maamuzi yanayowahusu na maendeleo ya sekta ya umma kwa ujumla.

Lengo la Sheria hii ni pamoja na kuwezesha kuundwa kwa Mabaraza ya Wafanyakazi mahali pa kazi yaani katika kila Wizara, Idara za Serikali Zinazojitegemea, Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Serikali za Mitaa na Wakala za Serikali. Nafurahi kusikia kuwa zoezi la uundaji wa Mabaraza ya Wafanyakazi katika mkoa wetu linatekelezwa vizuri. Kama zipo sehemu ambazo hazijaunda Mabaraza yao, hatua za makusudi zichukuliwe kwani kutofanya hivyo ni uvunjwaji wa sheria.

Uzoefu umeonyesha kuwa pale mabaraza haya yanapotumika vizuri yanasaidia sana kuleta maelewano mahali pa kazi. Kupitia mabaraza haya migomo ya wafanyakazi isiyo ya lazima imeweza kuepukwa na migogoro mingi imeshughulikiwa kwa njia ya majadiliano. Ni muhimu tukaendeleza utamaduni huu kama njia ya ustaarabu ya kudai maslahi badala ya migomo. Serikali kwa upande wake imeendelea kuwahakikishia kuwa itaendelea kuwahimiza waajiri kutoa fursa ya kujadiliana na wafanyakazi wake.

Kwa kupitia kikao hiki nawahimiza waajiri wote mkoani Kagera kuhakikisha kuwa madai mbalimbali ya watumishi yanashughulikiwa ipasavyo kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba mabaraza haya yanafanya vikao vyake inavyotakiwa kisheria.

Pamoja na umuhimu wa kumjali mtumishi, msisitizo uliopo hivi sasa serikalini na mahali pengine pa kazi ni pamoja na umuhimu wa watumishi hao kuongeza tija. Ikumbukwe kwamba bila watumishi kujituma zaidi na kuwa wabunifu ili kungeza tija, Serikali haiwezi kupata mapato ambayo yataiwezesha kuboresha maslahi ya Watumishi. Uboreshaji wa utumishi wa umma unaoendelea unasisitiza watumishi kuondokana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wafanye kazi kimkakati kwa kujali matokeo ya kazi. Lengo likiwa ni kutoa huduma bora na kuimarisha uwajibikaji wa serikali kwa umma.

Baraza la Wafanyakazi ni chombo muhimu sana katika kuleta tija mahali pa kazi. Nitafurahi iwapo mikakati ya kuongeza tija na kupunguza gharama za uendeshaji wa Sekretarieti itakuwa ni agenda ya kudumu katika mikutano ya Baraza hili.

Kwa mujibu wa Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma (Public Service Negotiating Machinery Act) Na. 19 ya mwaka 2003, Baraza hili la Wafanyakazi lina majukumu makuu yafuatayo:-

  • Kuwashirikisha wafanyakazi wa Serikali katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali;
  • Kuishauri Serikali juu ya ufanisi wa kazi, kushauri hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kutoa huduma bora kwa wananchi;
  • Kuishauri Serikali ili kuboresha maslahi ya wafanyakazi;
  • Kuishauri Serikali juu ya miundo na masharti ya utumishi (scheme of service) ;
  • Kupokea na kuthibitisha mipango na makisio ya mapato na matumizi ya Sekretarieti;
  • Kuishauri Serikali juu ya upandishwaji vyeo kwa watumishi na nidhamu kazini; na
  • Kujadili na kutoa ushauri kuhusu mipango ya elimu kwa wafanyakazi kwa ujumla na elimu kazini.

 

 

 

 

 

 

 

 
 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 

 

 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 
 
 
 

Picha ya pamoja ya baraza jipya la wafanyakazi lililozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa kagera Mh.Mohamed Babu. Waliokaa kutoka kushoto ni Katibu Tawala (M) Bw. Nassor Mnambila na katikati ni Mh. Mohamed Babu.

 

 

Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kupitia kumbukumbu za kazi za Baraza lililotangulia ili kujenga msingi wa kutekeleza majukumu yenu kwa ufanisi. Ni matumaini yangu pia Wajumbe watapata fursa ya kujifunza mambo mengi kuhusu majukumu haya kupitia mada zitakazowasilishwa.

Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu ningependa pia kuzungumza kwa kifupi mambo yafuatayo.

Jambo la kwanza ni ushabiki wa kisiasa mahali pa kazi. Sote tunafahamu kuwa kwa mujibu wa kanuni za maadili ya utumishi wa umma, ni kosa la kinidhamu na la kimaadili mtumishi wa umma kujihusisha na shughuli za kisiasa mahali pa kazi na wakati wa kazi.

Kwa hiyo, ni wajibu wa Baraza ili kuhakikisaha kuwa watumishi wenzao hawajihusishi na mambo ya siasa mahali pao pa kazi.

Jambo la pili ni janga la UKIMWI ambalo linatishia raslimali watu katika Taifa na Uchumi kwa ujumla. Tukipuuzia janga hili, nguvu kazi tunayoijenga itapotea na hivyo kudhoofisha uwezo wa Taifa wa kutoa huduma bora.

Lengo la Mkoa lilikuwa ni kupunguza kuenea kwa virusi vya UKIMWI kutoka asilimia 3.7 mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 1.8 mwaka 2010 . Mkoa umejitahidi kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka asilimia 3.7 mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 3.4 mwaka 2010 (takwimu zinazochukuliwa kwenye vituo, (Demographic Health Surveys) na asilimia kuanzia 5.5 hadi 9 mwaka 2010 (takwimu kutoka kwenye vitengo vya upimaji).

Hivyo, naomba kutumia fursa hii kuwaasa mjiepushe na vitendo vinavyosababisha na kuchochea ongezeko la UKIMWI.

Njia salama za kujikinga na virusi vya UKIMWI ni kama ifuatavyo:-

•  Kujiepusha kabisa kufanya vitendo vya ngono.

•  Kuheshimu na kufuata mafundisho ya viongozi wa madhehebu ya dini yanayokataza kujihusisha na vitendo vya ngono.

•  Kutumia kondomu kwa usahihi

Ndugu Wajumbe, napenda kuwakumbusha kuwa mwongozo wa kuhudumia watumishi waishio na virusi vya UKIMWI katika utumishi wa Umma uliotolewa uzingatiwe na kufuatilia utekelezaji wake kwa karibu zaidi kwani utumishi bila UKIMWI inawezekana.

Baada ya kusema haya, nafurahi kutangaza kuwa Baraza la Wafanyakazi katika Sekretarieti ya Mkoa wa Kagera, limezinduliwa rasmi, na nawatakia mafanikio katika shughuli zenu kwa kipindi chote mtakachokuwa wajumbe wa Baraza hili.

 

 

 
 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 
Habari mpya 7 [ Nyumbani ] au
Rudi juu
 
     
Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa KAGERA, BUKOBA, TEL: 028 - 2220215/17, FAX: 027-2752184