JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OFISI YA MKUU WA MKOA KAGERA
     
 
     
 
 
     
 
Ajira mpya [ Nyumbani ] au
 
 
 

OFISI YA MKUU WA MKOA WA KAGERA YAENDESHA KONGAMANO LA MIAKA HAMSINI (50) YA UHURU WA TANZANIA BARA NA KUTOKA NA MAAZIMIO KUMI NA TANO.

Katika kuadhimisha miaka hamsini (50) ya Uhuru wa Tanzania Bara, ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kagera iliandaa kongamano la wadau wa mkoa wa Kagera ili kujadili mstakabali wa mkoa wa Kagera kwa miaka hamsini ijayo ambapo kongamano hilo liliwahusisha wananchi wote wa mkoa wa Kagera.

Kongamano hilo lilifanyika tarehe 29/11/2011 katika ukumbi wa ‘'Linas Club'' ndani ya mji wa Bukoba na liliongozwa na mheshimiwa mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabiani I. Masawe aliyekuwa Mwenyekiti wa kongamano hilo. katika kongamano hilo zilitolewa mada tatu.

Mada ya kwanza ilikuwa ni “Huduma za jamii katika miaka hamsini ya Uhuru mkoa wa Kagera”, mada hii ilitolewa na Askofu Msaidizi Methodius Kilaini wa Kanisa Katoliki jimbo la Bukoba. Mada ya pili ilikuwa ni Uchumi na Uzalishaji katika miaka Hamsini ya Uhuru na ilitolewa na Jonas Kaleshu kutoka chuo kikuu cha Ushirika Moshi. Mada ya tatu ilitolewa na Liliani Lwakatare ambayo iligusia mwelekeo wa mkoa wa Kagera katika miaka hamsini ya uhuru ijayo. Mada hizo zote tatu zilijadiliwa na wananchi wote waliohudhulia katika kongamano.

Aidha katika majadiliano ya kongamano hilo, wadau waliweza kajadili kwa kina na kutoka maazimio kumi na matano ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi katika miaka hamsini ya uhuru ijayo na wananchi wa mkoa wa Kagera watakaokuwepo kwa kipindi hicho ili kuufanya mkoa wa Kagera kupiga hatua katika maendeleo ya Mkoa. Maazimio hayo ni kama ifuatavyo:

  • Watendaji wa serikali na mamlaka zinazohusika na utoaji wa huduma za jamii waache ukiritimba katika utekelezaji wa majukumu yao.
  • Kuhimiza Wanakagera walioko nje ya mkoa na wenye uwezo mzuri wa kiuchumi kurejea na kuwekeza nyumbani.
  • Wanakagera tujifunze kutumia fursa zilizopo za taasisi za fedha ili kupata mitaji kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
  • Wananchi wa Kagera kukubali mabadiliko na kuweka nguvu ya pamoja katika shughuli za uchumi, uzalishaji na kuchangia shughuli za maendeleo.
  • Mkoa upate taarifa “Database” ya Wanakagera walioko nje ya mkoa.
  • Serikali iwasaidie wananchi ili waweze kuongeza thamani ya mazao ya biashara kabla ya kuyauza katika soko.
  • Mkoa kusimamia utekelezaji wa sheria ya uzurulaji kwa vitendo pamoja na kuhimiza jamii kufanya kazi kwa bidii na maarifa zaidi.
  • Mkoa uhimize suala la michezo pamoja na kutenga maeneo ya michezo katika mipango ya maendeleo ya mkoa.
  • Mkoa usimamie kwa vitendo sheria ya kuhifadhi mazingira na kuhakikisha kwamba ujenzi wa viwanda na miundombinu mbalimbali unazingatia tathmini ya athari ya mazingira na tahadhari juu ya mabadiliko ya tabia nchi.
  • Vyombo vya Habari vilivyopo viandae “Documentary' katika wilaya zote za mkoa wa Kagera, kuonesha fursa zilizopo pamoja na shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofanyika katika mkoa wa Kagera.
  • Midahalo na makongamano ya kuhamasisha maendeleo ifanyike kuanzia katika ngazi ya chini (k.m. mtaa/kijiji) kwa kubainisha changamoto zinazowakabili, kutoa njia za ufumbuzi na kuweka hatua madhubuti za utekelezaji. Matokeo ya mihadalo/makongamano hayo yajadiliwe katika Kongamano la mkoa.
  • Mkoa uendelee kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika mkoa wa kagera ili kupata wawekezaji zaidi kwa lengo la kukuza wastani wa kipato cha mwanaKagera.
  • Wananakagera kuendelea kujenga tabia ya uzalendo kwa wananchi na kuanzia Utaifa wetu hasa kwa kudumisha heshima, umoja na amani.
  • Serikali ihamasishe na kuelimisha wananchi kuhusu dhana ya ufugaji wa samaki na umuhimu wake katika kulinda ziwa Victoria na kujiongezea kipato kwa mwananchi.
  • Mkoa kuweka kipaumbele katika huduma ya Afya ya msingi kwa kuwezesha jamii kutumia bima ya afya na kuongeza mapambano dhidi ya magonjwa ya Malaria, Ukimwi, Kisukari, Shinikizo la damu n.k.

Hapa juu kushoto ni Askofu Methodius Kilaini akifafanua jambo wakati wa kongamano, katikati ni Katibu Tawala wa Mikoa (M) Bw. Nassor Mnambila na kulia ni sehemu ya washiriki ambao walihudhuria katika kongamoto hilo.

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 

 

 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 
Ajira mpya [ Nyumbani ] au
Rudi juu
 
     
Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, BUKOBA, TEL: 028 - 2220215/17, FAX: 0282752184