Hali ya Mazingira ya Wilaya
Wilaya ya Biharamulo ina eneo la misitu ya asili lenye ukubwa wa hektari 163,945.83 na eneo la misitu ya hifadhi ya msitu uliopadwa ina ukubwa wa hektari 352.9 . Shuguli zinazofanyika katika maeneo haya ni pamoja na uvunaji wa mazao ya misitu kama vile mbao, asali.
Aidha uchimbaji wa madini ya dhahabu hufanyika katika maeneo ya Tulawaka (ambapo kuna Mgodi wa dhahabu), (maeneo ambayo yameathirika sana). Pia upo uchimbaji mdogo mdogo wa dhahabu unaofanyika katika maeneo ya Kata za Nyakahura na Kalenge.
Pia kumekuwa kukifanyika shughuli za upasuaji wa mbao isivyo halali kwa kukata miti ovyo, uchomaji ovyo wa mkaa, malisho ya mifugo ndani ya hifadhi na misitu ya asili kusipozingatia matumizi bora ya ardhi, kuendesha shughuli za kilimo katika misitu, ujangili, makazi ya watu kinyume na sheria pamoja na uchomaji moto misitu.
Athari za Uharibifu wa Mazingira
Kutokana na shughuli hizo zinazofanywa na binadamu zipo athari za dhahiri kama ifuatavyo:
Kutoweka au kupungua kwa kiwango kikubwa cha raslimali zilizopo kwa kutozingatia uvunaji endelevu.
Uharibifu mkubwa wa mazingira ambao unaweza kusababisha maeneo haya kugeuka jangwa
Uchafuzi wa vyanzo vya maji unaosababishwa na wachimbaji wa dhahabu kutumia maji ya mito kuoshea madini
Kutoweka kwa misitu kunakosababishwa na uchomaji moto misitu ovyo
Ardhi inayotumika kukosa rutuba kunakotokana na matumizi yasiyozingatia kanuni za kilimo bora.
Mikakati iliyowekwa na Wilaya kukabiliana na Uharibifu wa Mazingira
Katika kukabiliana na uharibifu huo, Wilaya imeweka mikakati ifuatayo ambayo inaendelea kutekelezwa:
Kuwaondoa wavamizi wafugaji na mifugo kwenye maeneo waliyovamia: “Operation” ya kuondoa mifugo katika misitu ya hifadhi na mapori imefanyika. Hii ikiwa ni pamoja na kuondoa na kurudisha mifugo kutoka nchi za jirani.
Kuendeleza njia za asili za hifadhi ya malisho kwa ajili ya mifugo: Katika hili misitu wa Lusahunga wenye ukubwa wa Hektari 4,000 umependekzwa kutangazwa kuwa misitu wa Halmashauri ya Wilaya ambao utakidhi shughuli za malisho wakati wa kiangazi.
Wilaya inaendelea kuendesha kampeni ya kupanda miti ambayo inaenda sambasamba na kampeini ya kuhifadhi misitu ya asili iliyopo: Katika utekelezaji wa hili jumla ya vikundi 47 na shule za Msingi katika kata 3 zimeanzisha vitalu vya miche ya miti. Pia jumla ya miti 3,000,000 imeshapandwa kwa kipindi cha Januari – Juni, 2007 kati ya hiyo iliyopona ni miti 1,860,500 sawa na 62% (survival rate).
Matumizi bora ya teknolojia ya nishati: Katika suala la kuhifadhi misitu, wilaya inaendeleza teknolojia ya matumizi bora ya nishati kwa kutengeneza majiko sanifu: Kazi hii ilienda sambasamba na kutoa mafunzo kwa mafundi 35 wa majiko sanifu katika wilaya. Hadi kufikia Juni, 2007 jumla ya majiko sanifu 15,023 yalikuwa yametengenezwa kwa ajili ya matumizi ya Wananchi. Hii ikiwa ni hatua mojawapo ya kupunguza uharibifu wa mazingira.
Kuweka taratibu madhubuti za uvunaji na kubaini wachomaji wa mkaa, wafanyabiashara na watumiaji wakubwa wa nishati ya kuni. Mpango wa uvunaji raslimali ya misitu wa wilaya umeandaliwa, Kamati ya Wilaya ya Uvunaji wa mazao ya misitu imeundwa na inafanya kazi.
Kufanya juhudi za ugani za kuendeleza na kusambaza matokeo yenye mafanikio ya nishati mbadala. Wachoma mkaa 33 wamehamasishwa na kuelekezwa kuchakata mkaa kwa kutumia matanuru ya ardhini (earth kiln).
Kubainisha vyanzo vyote vya maji na hali ya mazingira yake kwa lengo la kurahisisha utekelezaji wa usimamizi wa mazingira. Maeneo yamebainishwa katika vijiji vyote 49 vya Wilaya, na miti 342 rafiki kwa vyanzo vya maji imepandwa. Hii ni pamoja na kubainisha aina ya miti inayofaa kupandwa katika maeneo mbalimbali ya vyanzo vya maji.
Kuwa na Mpango kamambe wa matumizi bora ya ardhi uwe umehuishwa na kusambazwa vijijini. Mafunzo juu ya matumizi bora ya ardhi yametolewa katika vijiji 22 na vijiji 6 vimeshandaa mpango kamambe wa matumizi bora ya ardhi. Hii ni pamoja na kuandaa Programu ya Hifadhi ya Mazingira.
Kuwajibisha Uongozi wa eneo husika utakaoshindwa kutekeleza zoezi la kudhibiti matukio ya moto katika maeneo yao. Viongozi wa ngazi zote wameshaelekezwa juu ya suala hili.
Kuandaa tuzo ya kupanda na kutunza miti kwa taasisi, mashirika na watu binafsi: Tuzo ya Wilaya ya kuhifadhi vyanzo vya maji na upandaji wa miti imeanzishwa na washindi watakuwa wanapewa tuzo siku ya upandaji miti kiwilaya.
Kuendelza ufugaji nyuki endelevu. Sekta ya nyuki imekuwa ikitoa huduma kwa wafugaji nyuki kwa kutoa mafunzo yahusuyo mbinu za kisasa za ufugaji nyuki pamoja na urinaji asali salama. Kwa kushirikiana na mradi wa CHEMA vikundi vya wafugaji nyuki vimepewa zana bora za kisasa za kuwasaidia katika shughuli za utengenezaji wa mizinga ya kisasa na urinaji zinazolinda usalama wa mazingira.
Operesheni ya kukamata mkaa, kuni na mbao inaendelea kufanyika na wahusika kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
|