JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OFISI YA MKUU WA MKOA KAGERA
     
 
     
 
 
     
JAMII, JINSIA NA WATOTO
 
Jamii [ Jinsia ] [ Watoto ] [ Nyumbani ] au
 
 

MAENDELEO YA JAMII

 

Lengo kuu la sekta ya Maendeleo ya Jamii ni kuchukua hatua zinazowawezesha watu kutambua uwezo walio nao wa kubaini matatizo na uwezo wao wa kutumia raslimali zilizopo kujitatulia matatizo hayo, kujipatia na kujiongezea kipato na kujiletea maisha bora zaidi na hivyo kujiletea maendeleo, na kuweka mazingira muafaka yatakayo wawezesha wanawake na wanaume kutekeleza majukumu yao katika jamii kwa kuzingatia mahitaji ya kijinsia. Aidha lengo jingine ni kuongeza ushirikishwaji wa wanawake na vijana katika shughuli za maendeleo, hatimaye kuleta maisha bora kwa kila mtanzania.

Kazi zinazotekelezwa na sekta ya Maendeleo ya Jamii katika mkoa wa Kagera ni pamoja na:-

•  Kujenga uelewa wa wananchi ili aweze kushiriki shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo yao kwa njia ya kujitegemea na kuwasaidia kupanga mipango inayotekelezeka.

•  Kuhamasisha wananchi kujiunga katika vikundi vya kijamii na SACCOS ili kuanzisha na kutekeleza shughuli za uzalishaji mali zenye kuchangia kuinua hali zao za maisha, pamoja na utoaji wa mikopo ya kiuchmi kwa wananwake kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii wa wanawake.

•  Kushirikisha jamii katika mapambano dhidi ya janga la UKIMWI na kutoa msaada kwa watoto yatima.

•  Kusaidia jamii jinsi ya kuondokana na mila potofu zinazochangia kuzorotesha maendeleo ya wananchi.

TATIZO LA UKIMWI:

Kama inavyoeleweka mgonjwa wa kwanza wa Ukimwi alipatikana katika kijiji cha kashenye kata kashenye wilaya ya misenyi hapa mkoani Kagera. Ilikisiwa kuwa kuna sehemu zenye maambukizi makubwa ya virusi vya UKIMWI katika maeneo yenye mikusanyiko mingi ikiwemo katika jamii ya wavuvi katika visiwa vya Wilaya ya Muleba na katika mwambao wa ziwa victoria, tatizo la UKIMWI Katika Mkoa wa Kagera linaendelea kupungua kutokana na wanachi kuelewa chanzo na maeneo ambayo ni tete kwa ajili ya maambukizi. Mkoa kwa kutumia gari la sinema umeweza kuhamasisha na kutoa mafunzo kwa njia ya sinema kama ifuatavyo:-

WATU WALIOHUDHURIA KWENYE SINEMA

WILAYA

2009

2010

2011

Bukoba H/M

209

301

271

Muleba

865

1,233

1,914

Karagwe

720

814

1,121

Misenyi

1,600

2,719

2,030

Ngara

1,218

899

1,300

Biharamulo

1,677

1,820

537

Bukoba H/W

1,009

872

988

Chato

1,400

1,345

2,539

Hali hii inadhihirisha yafuatayo: -

•  Matumizi ya kondomu yamepanda kutokana na kwamba kila mahali sinema ilipoonyeshwa tuliweza kugawa kondom na jumla ya mabokisi 200 yenye kondomu 100 kila moja yaligawiwa kwa wananchi,18,569 wengi wao wakiwa vijana. Aidha, kinamama walijitokeza kwa wingi kuchukulia wenzi wao kondom. sinema ilisababisha wakati wa usiku idadi ya wanaopima afya zao kuongezeka na kuwa kubwa ikilinganishwa na wakati wa mchana hayo yalisemwa na mpimaji kutokana na takwimu alizozipata na kama inavyoonyeshwa hapo chini kwenye jedwali:-

Na.

HALMASHAURI

WALIOPIMA

WALIOKUTWA NA MAAMBUKIZI

1

Bukoba H/M

672

3

2

Bukoba H/W

320

1

3

Karagwe

540

2

4

Chato

789

2

5

Misenyi

685

6

6.

Muleba

528

8

7.

Ngara

380

2

8

Biharamulo

430

2

•  Takwimu hizo zinaonyesha kwamba wananchi wengi hupendelea kupima afya zao wakati wa usiku na wako tayari kuchukua majibu yao bila woga pamoja na uhamasishaji kwa njia ya sinema. Mkoa unatumia gari hilo kuhamasisha dhana ya kilimo kwanza ili kuendeleza mapinduzi ya kijani katika mkoa.

•  Watu wengi wameonyesha kujali maisha yao na kuacha ngono za holela.

•  Gari la sinema limekuwa kichocheo cha wananchi wengi kubadili tabia na kuacha mila potofu za kujamiiana.

•  Shule za sekondari 10 zimehamasishwa kwa njia ya sinema ili wanafunzi waache mapenzi wawapo masomoni na kivutio kikubwa ni sinema ya ZAWADI ambayo imewavutia wanafunzi wengi.

•  Shule za sekondari 40 zimehamasishwa kuhusu janga la UKIMWI na wanafunzi wameanzisha klabu za kupinga na kudhibiti UKIMWI katika shule zao. Aidha, wanafunzi wameanzisha maktaba za kuzuia UKIMWI na kukomesha mimba za utotoni.

Wilaya ya Muleba inaongoza, kwa kuwa na maambukizi makubwa ya UKIMWI kutokana na hali ilivyo huko visiwani. Bado jamii ya wavuvi inaendelea na tatizo la kuwa na ngono za mnada kwamba mwenye fedha nyingi ndiye anayefanya mapenzi na mwanamke mzuri na ambaye ni mgeni katika maeneo ya visiwani. Hii imetokana na utafiti wa shirika lisilo la kiserikali la ADRA na TANESA.

WATOTO YATIMA NA WAISHIO KATIKA MAZINGIRA HATARISHI

Mkoa una jumla ya watoto 85,594 ambao wamebainishwa katika Halmashauri za Mkoa wa Kagera, kati yao watoto wa kiume 23,338 na wa kike 23,038 wanahudumiwa na mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo husaidia kutoa huduma mbalimbali za kuwaendeleza watoto hao. Mashirika hayo ni TADEPA,MAPEC, WAMATA,KARADEA,SAWAKA,WOMEDA,WVT,HYAWA RC, ELCT, HUMULIZA, MATUMAINI MAPYA UNICEF na mashirika mengi yaliyopo hapa Mkoani. Takwimu hizo ni kwa watoto wanaohudumiwa na mashirika yasiyo ya kiserikali kama zinavyoonyeshwa katika jedwali lifuatalo hapo chini:-

Na

HALMASHAURI

ME

KE

JUMLA

1.

Ngara

3,118

3,062

6180

2.

Misenyi

4,585

4,671

9256

3.

Karagwe

3,515

3,415

6,930

4.

Bukoba H/M

844

1,105

1,949

5.

Muleba

12,905

12,455

25,360

6.

Chato

7,600

7,252

14,852

7.

Bukoba H/W

9,021

8,210

17,231

8.

Biharamulo

2,055

1,781

3,836

 

JUMLA

43,643

41,951

85,594

Kazi zingine zinazotekelezwa na sekta ya Maendeleo ya Jamii katika mkoa wa Kagera ni pamoja na:-

•  Kujenga uelewa wa wananchi ili waweze kushiriki shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo yao kwa njia ya kujitegemea na kuwasaidia kupanga mipango inayotekelezeka kwa kutumia mbinu shirikishi ya O & OD.

•  Kuhamasisha wananchi kujiunga katika vikundi vya kijamii na SACCOS ili kuanzisha na kutekeleza shughuli za uzalishaji mali zenye kuchangia kuinua hali zao za maisha, pamoja na utoaji wa mikopo ya kiuchumi kwa wanawake kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii wa wanawake.

•  Kusaidia jamii jinsi ya kuondokana na mila potofu zinazochangia kuzorotesha maendeleo ya wananchi. Aidha, tatizo la unyanyasaji wa wanawake na watoto linaendelea kufanyiwa kazi na idara ya maendeleo ya Jamii

•  Wananchi wameelimishwa katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutambua fursa au rasilimali walizo nazo katika kujiletea maendelo yao , pamoja na kutambua vikwazo watumiapo rasilimali hizo(mafunzo ya O&OD yametolewa kwa asilima 98.

•  Sekta ya maendeleo ya jamii inaendelea kuwa chachu katika kuhamasisha na kuwajengea uwezo wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu katika uanzishaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Miradi iliyotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa shule za Sekondari za Kata, Barabara za jamii vijijini, mikopo kwa kina mama na vikundi vya wajasiliamali (USHIRIKA), uundaji au uanzishaji wa vikundi vya kijamii (CBOs) pamoja na vikundi vya kinamama.

Utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake kwa lengo la kuinua mapato yao na kujiletea maisha bora.

•  Sekta ya maendeleo ya jamii inaendelea kuhamasisha wananchi kuhusiana na uundaji wa vikundi vya kijamii, na uanzishaji wa SACCOS katika maeneo wanakoishi na sehemu za kazi kama njia ya kuunganisha nguvu zao pamoja na kutumia fursa zilizopo kupitia malengo (2) mawili ya MKUKUTA ili kupambana na umasikini wa kipato na kujiletea maisha bora.

•  Sekta ya maendeleo mkoani Kagera imekuwa mstali wa mbele kuhamasisha na kuzishauri Halmashauri za Wilaya na manispaa kutoa mchango wa asilimia 5% ya mapato ya Halmashauri katika mfuko wa Maendeleo ya Jamii ili uwe mfuko endelevu, na kuwawezesha kinamama kumiliki mali na kushiriki kuchangia pato la kaya na jamii kwa ujumla.

•  Aidha sekta ya maendeleo ya jamii kwa kushirikiana na sekta mbalimbali hususan sekta ya Ushirika, Kazi na Vijana hutoa mafunzo kwa wajasiliamali wadogo wadogo kuwapatia elimu na maarifa yatakayowawezesha kuhimili biashara za ushindani katika mazingira yao ya soko huria na utandawazi.

 

 

 
 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 

 

 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 
 
 

WATOTO

•  Kumekuwepo na ongezeko kubwa la watoto yatima na waishio katika mazingira magumu. Jambo hili limekuwa tatizo kubwa na kusababisha watoto kuhama kutoka vijijini na kuja kuishi mijini. Jambo hili limesababisha watoto kwenda katika vituo mbalimbali vya kulelea watoto yatima na wengine kuishi mitaani.

•  Mikakati inayotumika kukabiliana na tatizo hilo ni kufanya uchambuzi wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwa ushirikiano na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kama World Vision Tanzania, HUMULIZA, HUYAWA, PACT – Tanzania pamoja na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali.

•  Mchakato wa kuwatambua watoto walio katika mazingira magumu unaendelea katika wilaya za Ngara, Biharamulo na Chato. Uchambuzi unapokamilika takwimu za watoto waliotambuliwa hukabidhiwa katika halmashauri husika na baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) yanazoweza kutoa msaada kwa watoto hao. Mfano mzuri ni Asasi ya Humuliza inayosaidia watoto hao wakiwa katika maeneo walikozaliwa. Humuliza huwasaidia watoto kwa kuwajengea nyumba za gharama nafuu kwa kutoa bati, milango, madirisha na ujenzi hufanywa na jamii ya vijiji husika.

•  HUMULIZA pia husaidia miradi kama ufugaji wa ng'ombe au mbuzi wa maziwa kwa watoto hao ili waweze kumudu maisha wakiwa huko huko walikozaliwa. Kwa ujumla hii ndiyo njia ambayo mkoa unahimiza katika kuwalea na kuwatunza watoto yatima na walio katika mazingira magumu.

•  Sekta ya maendeleo ya jamii inasaidia jamii jinsi ya kuondokana na mila potofu hasa za kurithi wajane waliofiwa na waume zao pamoja na kusaidia jamii jinsi ya kubadili tabia.

•  Mafunzo yametolewa kwa wananchi 877 kuhusu athari za kuendeleza tabia mbaya ya kuendeleza ngono zembe na kurithi wajane au wagane ambao vifo vya wenzi wao vimetokana na ugonjwa wa UKIMWI.

DAWATI LA JINSIA

Kila Halmashauri katika mkoa wa Kagera ina dawati la jinsia na kwa kuzingatia msimamo wa nchi yeti kuhusu usawa wa kijinsia Halmashauri zote zimekuwa na msimamo wa kutekeleza maazimio mbalimbali ambayo Serikali imekuwa ikisaini mikataba yake. Mfano azimio la haki za binadamu la mwaka 1948 la kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake (CEDAW 1979) pamoja na maazimio mbali mbali yanayohusu haki za wanawake na watoto.

Madawati haya yamekuwa chachu ya kuleta usawa katika utendaji kazi na umiliki wa rasilimali katika jamii ikiwa ni pamoja na kuachana na mila potofu zinazosababisha wananwake kuonewa na kupuuzwa kutokana na kutokuwa na kauli ya kumiliki mali. Aidha, katika Mkoa wa Kagera wanawake watatu (3) wamerudishwa katika makazi yao baada ya kufukuzwa na jamaa wa marehemu waume zao kwa sababu ya mila na destuli kwamba mara mwanamke anapofiwa hastahili kuendelea kumiliki mali za marehemu mume wake.

MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI

Idara ya maendeleo ya jamii inaratibu mashirika yasiyo ya kiserikali yapatayo 115, ambayo yanafanya kazi katika Halmashauri za wilaya katika mkoa wa Kagera. Aidha, Idara pia inasaidia mashirika yasiyo ya kiserikali kuandikishwa na kupata hati zao za usajili.

Changamoto zinazoikabili idara ya maendeleo ya Jamii Mkoani.

Zipo changamoto mbalimbali zinazosababisha vikwazo mbalimbali katika utekelezaji wa kazi za idara kama ifuatavyo:-

•  Tatizo la usafiri kwa watumishi walioko kwenye kata pamoja na Halmashauri nyingi kukosa vyombo vya isafiri.

•  Tatizo la makazi kwa watumishi waishio kwenye kata.

•  Tatizo la vitendea kazi.

•  Ukosefu wa ofisi kwa watumishi katika kata.

•  Fedha za matumizi ya kawaida zinazoletwa na serikali kufanyia kazi ni kidogo kwa ajili ya kazi za idara ya maendeleo ya jamii.

•  Mashirika yasiyo ya kiserikali kutotoa taarifa zao za utendaji kazi kwa wakati.

Jinsi ya kukabiliana na changamoto

•  Wizara ishirikiane na OWM TAMISEMI kusaidia kutoa vyombo vya usafiri kwa watumishi wa maendeleo ya Jamii katika ngazi zote Wilayani na kwenye kata.

•  Watumishi wa sekta ya maendeleo ya jamii kwa kushirikiana na wananchi wanatoa hamasa kwa wananchi waweze kujitolea kuwajengea nyumba watumishi wao wa sekta zote.

•  Wakurugenzi wa halmashauri wanahimizwa kuchangia katika OC ya Idara ya maendeleo ya jamii ili kuifanya idara hii iweze kufanya kazi zake vizuri.

•  Mkoa na halmashauri zinafanya jitihada ya kuwawezesha watumishi wa maendeleo ya jamii kuwafikia walengwa..

•  Mashirika yasiyo ya kiserikali yamekumbushwa kuwasilisha taarifa za kazi zao katika mamlaka ya serikali za mitaa.

•  Uanzishaji wa mitandao ya mashirika yasiyo ya kiserikali ya mkoa na wilaya imesaidia kusukuma utendaji wa kazi za mashirika hayo.

Vyuo vya Maendeleo ya wananchi

Mkoa una vyuo vya Maendeleo ya wananchi 3 ambavyo ni kama ifuatavyo:-

•  Gera kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi.

•  Rubondo kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo.

•  Ilemela Kilichopo Katika Halmashauri ya Wila ya Ngara.

Vyuo hivi ni chachu ya maendeleo ya Jamii katika maeneo vilipo lakini vyuo hivi vimekuwa vikitumia zana duni sana hasa kwenye useremala, ushonaji, uhunzi, uchomeleaji wa vyuma, udereva, ufundi magari na uashi. Serikali ichukue hatua ya kuvifanya kama vyuo vya VETA vinavyoendeshwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi ili viweze kuwa kivutio kwa vijana wengi wanaomaliza elimu ya sekondari na msingi. Aidha Wizara ya jamii jinsia na watoto iongeze walimu wenye sifa katika fani mbalimbali katika vyuo vya maendeleo ya wanachi watakaowezesha uwepo wa wataalam vijijini wanaotoka katika vyuo hivi.

Kilimo kwanza

Idara ya Maendeleo ya Jamii inashiriki kikamilifu katika uundaji wa vikundi vya vijana ambao wanajishughulisha na kilimo ili waweze kutumia zana za kisasa za kilimo kama matrekta madogo (Power Tillers). Hadi sasa vikundi 57 vya vijana vimeundwa kwa lengo la kuboresha kilimo cha mazao mbalimbali ikiwemo mpunga, mahindi, mhogo na migomba mkoani. Halmashauri za wilaya zinaendelea kuhamasisha vijana kujiunga na SACCOS pamoja na vikundi mbalimbali ili viweze kutafuta mikopo kwa ajili ya kuendeleza sekta ya kilimo katika maeneo ya vijijini.

 

 

 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
     
     
 
     
Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, BUKOBA, TEL: 028 - 2220215/17, FAX: 028-2752184