JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OFISI YA MKUU WA MKOA KAGERA
     
 
     
 
 
     
KILIMO
 
[ Mifugo ] [ Nyumbani ] au
 
 
Utangulizi
 

Mkoa wa Kagera una eneo la hekta 1,593,758 zinazofaa kwa ajili ya kilimo. Hekta hizo kwa kila wilaya ni kama ilivyooneshwa kwenye jedwali lifuatalo hapo chini.

 

Eneo la Kilimo

Wilaya

Eneo la wilaya (Ha)

Eneo linalofaa kwa Kilimo (Ha)

Eneo (Ha) linalolimwa

% ya eneo linalolimwa (Ha)

BUKOBA MANISPAA

8,000

4,200

2,400

57

BUKOBA VIJIJINI

291,600

107,174

62,160

58

MISSENYI

270,875

99,726

57,840

58

MULEBA

1,073,900

288,000

143,137

49.7

BIHARAMULO

562,700

253,215

63,304

25

CHATO

357,200

267,900

99,123

37

NGARA

374,400

303,483

56,210

18.5

KARAGWE

771,600

270,060

190,000

70.3

JUMLA

3,710,275

1,593,758

674,174

46.7

 

 

Karibu asilimia 70 ya wakazi wa mkoa wa Kagera ambao kwa mwaka 2008 wanakadiriwa kufikia 2,502,000 hutegemea kilimo kukidhi mahitaji yao ya chakula na pia kama chanzo cha mapato.

Mazao muhimu ya chakula ni ndizi, mahindi, muhogo, viazi vitamu na maharage, ambapo mazao makuu ya biashara ni kahawa, pamba na chai.

 
 
Uzalishaji Msimu 2007/2008
 

Katika msimu wa kilimo ulioishia Juni 2008 Mkoa ulijiwekea lengo la kulima na kutunza hekta zipatazo 735,200 za mazao mbalimbali zilizotarajiwa kuzalisha tani 1,209,900 za ndizi, tani 236,400 za nafaka, tani 110,600 za mikunde, tani 854,100 za mazao ya mizizi, tani 53,450 za Kahawa maganda, tani 80 za tumbaku, tani 25,110 za Pamba mbegu, na tani 4,800 za majani mabichi ya chai.

Hadi kufikia Juni 2008 inakadiriwa kuwa Mkoa ulilima na kutunza hekta zipatazo 634,280 za mazao mbalimbali sawa na asilimia 86 ya lengo na kuzalisha jumla ya tani 2,245,200 za mazao ya chakula na jumla ya tani 46,120 ya mazao ya biashara kama inavyoneshwa kwenye jedwali hapa chini.

Uzalishaji wa Mazao ya Kilimo Msimu 2007/2008

 

ZAO

LENGO LA UZALISHAJI (M.T.)

 

UZALISHAJI (M.T.)

 

ASILIMIA

MAZAO YA CHAKULA

 

 

 

1. Ndizi

1,209,952

1,402,259

116

2. Mazao ya Nafaka

236,400

215,223

91

3. Mazao ya Mikunde

110,600

167,872

151

4. Mazao ya Mizizi

854,100

459,845

54

JUMLA MAZAO YA CHAKULA

2,411,052

2,245,199

na

MAZAO YA BIASHARA

 

 

 

1. Kahawa

53,450

32,361

60.5

2. Tumbaku

115

153.6

134

3. Pamba

25,110

8,820

35

4. Chai

4,800

4,889

102

JUMLA MAZAO YA BIASHARA

83,440

46,124

 

 

 
 
 

 

Sababu za Kutofikia Malengo kwa Baadhi ya Mazao
 

Uzalishaji wa pamba ulikuwa mdogo kwa sababu mvua za Vuli zilinyesha kwa wingi na kusababisha udongo katika maeneo yanayozalisha zao hilo kulowa maji. Pamba yote iliyopandwa mapema ilidumaa na kusababisha mavuno kupungua. Kwa zao la muhogo bado ugonjwa wa batobato kali anaathiri uzalishaji katika maeneo kadha

Kilimo cha Umwagiliaji

Mkoa wa Kagera una mabonde kadha yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji lakini bado kilimo hiki kinatekelezwa katika kiwango kidogo. Maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji wa maji kujitiririsha yenyewe (gravity irrigation) mkoani Kagera yanakadiriwa kuwa na ukubwa wa hekta zipatazo 10,400. Bonde kubwa kuliko yote ni la Mto Ngono ambalo huanzia wilayani Muleba kwa upande wa Kusini na kuishia wilaya ya Missenyi kwa upande wa Kaskazini. Hali ya kilimo cha umwagiliaji mkoani Kagera ni kama ifuatavyo:

Umwagiliaji Mashamba Mkubwa

Kampuni ya Sukari ya Kagera (Kagera Sugar) iliyoko wilaya ya Missenyi ndiyo pekee yenye kilimo kikubwa cha umwagiliaji. Shamba hili liko nje ya mabonde yanayoweza kutumika kwa umwagiliaji wa maji ya kujitiririsha yenyewe. Kampuni hiyo inalima hekta 7,500 za miwa na zote zinamwagiliwa maji kwa kutumia mifumo miwili ya unyunyiziaji maji. Hekta 4,000 zinamwagiliwa maji kwa mitambo inayotambaa ardhini (Central Pivot Irrigation System) na hekta 3,500 zinamwagiliwa maji kwa “Mobile Jet Guns na Sprinkler System”. Kampuni hiyo inaendelea kutayarisha shamba lingine la miwa la hekta 2,500 ambalo pia litakuwa likimwagiliwa maji.

Umwagiliaji wa Vikundi

Vikundi vya wakulima na wakulima binafsi wachache hutumia maji ya Mto Ngono kumwagilia hekta 32 za mashamba katika eneo la Mradi wa Umwagiliaji wa Nkenge wilayani Missenyi.

Umwagiliaji wa Asili

Wilayani Ngara kuna jumla ya hekta 3,000 zinazolimwa kwa umwagiliaji wa asili ( traditional irrigation ) unaofanyika katika mabonde mengi madogo madogo kwa kutumia maji ya vijito na mito midogo.

Sababu za Kilimo Duni cha Umwagiliaji

Wakulima walio wengi mkoani Kagera hawana utamaduni wa kumwagilia mazao yao kwa sababu sehemu kubwa ya mkoa hupata mvua za uhakika katika misimu yote miwili ya mwaka, yaani Masika na Vuli.

 
 
Upatikanaji wa Chakula Msimu 2007/08

Ilikadiriwa kuwa mwaka 2007 idadi ya wakazi wa mkoa wa Kagera ilikuwa 2,292,340 . Mahitaji ya chakula kwa wakazi wa mkoa huu kwa mwaka 2007/08 yalikuwa tani za metriki 627,530 za wanga na tani za metriki 62,750 za mikunde.

Chakula cha kutosha kilipatikana mkoani kote na ziada iliendelea kutumika hadi msimu wa Vuli 2008 na wakulima waliuza kiasi kingine kwa ajili ya kujipatia kipato. Hali ya chakula katika msimu wote wa kilimo 2007/2008 ilikuwa nzuri.

Ununuzi wa Mazao ya Biashara 2007/2008

Hadi 30 Juni 2008 jumla ya tani 22,500 za Kahawa ( Maganda ) zenye thamani ya shilingi bilioni 15.75 na tani 6,200 za Pamba Mbegu zenye thamani ya shilingi 1,895,587,100/= zilikuwa zimenunuliwa. Aidha tani 153.6 za Tumbaku zenye thamani ya TSh 212,729468/= na tani 4,380 za majani mabichi ya Chai zenye thamani ya Tshs 438,724,000/= zilikuwa zimenunuliwa.

  Malengo ya Kilimo Msimu 2008/2009

Katika msimu wa kilimo 2008/2009 mkoa umepanga kulima na kutunza jumla ya hekta 828,740 za mazao mbalimbali ya chakula zinazotarajiwa kuzalisha jumla ya tani 1,270,210 za ndizi, tani 399,670 za nafaka, tani 95,670 za mikunde na tani 1,526,625 za mazao ya mizizi.

Aidha, mkoa umelenga kulima na kutunza jumla ya hekta 171,410 za mazao mbalimbali ya biashara zinazotarajiwa kuzalisha jumla ya tani 57,310 za kahawa, tani 120 za tumbaku, tani 99,415 za Pamba mbegu, tani 5,170 za majani mabichi ya Chai na tani 13,145 za Mtama pombe.

 

Makadirio ya Mahitaji ya Chakula Msimu 2008/09

 

Inakadiriwa kuwa mwaka 2008 idadi ya wakazi wa mkoa wa Kagera imefikia 2,453,406 (maoteo). Mahitaji ya chakula kwa wakazi wa mkoa huu kwa mwaka 2008/09 ni tani za metriki 651,400 za wanga na tani za metriki 65,140 za mikunde.

Hadi mwisho wa Oktoba 2008 Wilaya zote ziliripoti kwamba chakula kilikuwa kinapatikana kwa kiwango cha wastani. Inatarajiwa kwamba katika msimu wa kilimo 2008/2009 mkoa utaweza kujitosheleza kwa chakula, endapo mvua zitanyesha kwa kiwango cha kawaida kama ilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Maandalizi ya Ununuzi wa Mazao ya Biashara 2008/09

Kwa kawaida ununuzi wa mazao mkoani hutegemea sana vyama vya vikuu vya ushirika ambavyo ni Kagera Cooperative Union (KCU), Karagwe Cooperative Union (KDCU), Biharamulo Cooperative Union (BCU) na Ngara Farmers Cooperative Society. Aidha ununuzi unafanywa na makampuni na vikundi vya watu binafsi.

Katika msimu wa ununuzi 2008/09 Vyama Vikuu vya Ushirika viwili na kikundi kimoja cha wakulima wanajishughulisha na ununuzi wa mazao katika wilaya mbalimbali. Aidha makampuni tisa ya binafsi yameruhusiwa kununua kahawa katika wilaya za Bukoba, Missenyi, Muleba, Ngara na Karagwe. Makampuni sita ya binafsi yameruhusiwa kununua pamba wilayani Biharamulo na Chato. Ununuzi wa zao la tumbaku utaanza mwezi Aprili 2009; na Tanzania Leaf Tobacco Company (TLTC) yenye makao yake mjini Kahama.

Ununuzi wa Mazao ya Biashara Hadi Oktoba 2008

Mwanzoni mwa msimu wa ununuzi 2008/2009 bei za Kahawa m aganda kwa wanunuzi walio wengi walianzia kwenye wastani wa TShs 800/= kwa kilogramu. Kwa wanunuzi wa zao la pamba bei ya wastani ilikuwa ni TSh 400/= kwa kilo.

Hadi 31 Oktoba 2008 jumla ya tani 48,038 za Kahawa maganda zenye thamani ya Tshs. 37,407,451,120/= zilikuwa zimenunuliwa mkoani kote. Aidha hadi 31 Oktoba 2008 Pamba mbegu Tani 6,500 zenye thamani ya TSh 2,600,000,000/= zilinunuliwa.

Changamoto

Sekta ya kilimo mkoani Kagera inakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na:

•  Magonjwa hatari ya mimea ambayo ni mnyauko bakteria wa migomba (Banana Xanthomonas Wilt), mnyauko fuzari wa kahawa (Coffee Fusarium Wilt), ugonjwa wa michirizi ya kahawia (Cassava Brown Streak Disease) na batobato kali ya mhogo (Cassava Mosaic Disease – UgVariant).

•  Idadi ndogo ya Maafisa Ugani isiyokidhi mahitaji. Hadi Oktoba 2008 Mkoa ulikuwa na jumla ya Maafisa Ugani 148 katika Halmashauri zake na kati ya hao 123 wako katika ngazi za Kata na Vijiji.

•  Vijana wengi wanaoishi vijijini wanashughulika na biashara ndogondogo badala ya kushiriki katika kilimo na wengine wanahamia mijini na hivyo kupunguza nguvukazi vijijini.

•  Wakulima kutumia pembejeo za viwandani kwa kiwango kidogo.

•  Kushuka kwa bei ya kahawa katika soko la dunia ambako kumesababisha bei ya Kahawa ishuke pia Mkoani.

Mikakati ya Kuendeleza Kilimo

Katika kupambana na changamoto zilizotajwa hapo juu Mkoa umeweka mikakati mbalimbali ya kuongeza uzalishaji wa mifugo na kilimo. Mikakati hiyo ni pamoja na:-

•  Kutumia sheria ndogo zilizopo katika Halmashauri za wilaya kuwabana na kuwawajibisha vijana wavivu.

•  Viongozi kuwajibika kwa kuyafanya mashamba yao kuwa ya mifano ya kilimo bora chenye tija.

•  Kuhimiza kilimo cha wanyamakazi zaidi kwenye maeneo yanayofaa kwa kilimo hicho hususan wilaya za Chato, Biharamulo na Missenyi.

•  Kuendeleza shamba la Kikulula la uzalishaji wa punda ambalo kwa sasa lina punda 130.

•  Kusimamia ufufuaji wa mashamba ya mazao ya biashara yaliyotelekezwa katika kila Halmashauri.

•  Kila Mtaalam wa Ugani kuwa na mpangokazi wa mwaka mzima kwa kutumia Daftari la Bwanashamba ili kuongeza uwajibikaji.

•  Kutumia kikamilifu mbegu bora za muhogo zinazozalishwa kwenye mashamba ya mbegu yaliyopo mkoani. Zipo jumla ya hekta 90 za mashamba mama ya kuzalisha mbegu ya mihogo inayovumilia batobato kali, zenye uwezo wa kuzalisha pingili milioni 27  kwa mwaka.

•  Kuhimiza na kuongeza matumizi ya aina mpya za migomba inayovumilia mashambulizi ya wadudu, migomba inayozalishwa katika mashamba ya Kyakailabwa, Nshambya na ARDI Maruku (Bukoba); Nkwenda (Karagwe) na Muleba. Aina hizi ni FHIA 17, FHIA 23, FHIA 25 na Yangambi Km5.

•  Kuzalisha miche bora ya kahawa kwenye bustani mama mbili za Ibwera (Bukoba) na Biirabo (Muleba) zenye uwezo wa kutoa jumla ya miche 720,000 aina ya kolona kwa mwaka. Aidha kila Halmashauri ya wilaya imeanza kuanzisha bustani za miche itokanayo na mbegu katika maeneo yanayofaa.

•  Halmashauri kwa kushirikiana na TaCRI na Vyama Vikuu vya Ushirika zitaendelea kununua mbegu bora za mazao na kuzisambaza kwa wakulima.

•  Kuunda “task forces” katika kila kijiji chenye ugonjwa wa Mnyauko bakteri wa migomba ili kuhakikisha ung'oaji wa migomba iliyougua unakamilika katika kipindi kifupi.

•  Kuhimiza vyama vikuu kuendelea kununua Kahawa na kutoa hamasa kwa wananchi kuendelea kutunza zao la kahawa, hata baada ya bei kushuka.

 

 
 
 
 

 

 

 
 
 
 

 

 
 
 

 

 

 
 
 

-

 
     
     
 
     
Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, BUKOBA, TEL: 028 - 2220215/54236-7, FAX: 027-2752184