JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OFISI YA MKUU WA MKOA KAGERA
     
 
     
 
 
     
 
 
[Kilimo ] Mifugo < Mada [ Nyumbani ] au
 
 
SEKTA YA UVUVI
 

Sekta ya Uvuvi ni moja ya Sekta muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii mkoani Kagera. Uvuvi katika Mkoa wa Kagera unafanywa katika maziwa, mito na mabwawa, Ziwa Victoria na maziwa mengine madogo ambayo ni Ziwa Ikimba, Burigi, Melula, Katwe, Luko, Karenge, Rushwa na Mitoma. Aidha mito inayochangia shughuli za Uvuvi ni mto ngono, kagera, kyabakumba, kyambu, kitokozi na mingine midogomidogo ambayo yote hupeleka maji katika ziwa Victoria . Kutokana na kuwepo kwa fursa nyingi, vatu wananchi wengi hujishughulisha na kazi za uvuvi kwa ajili ya kupata mahitaji yao ya kila situ.

Hata hivyo changamoto kubwa katika Sekta hii ni uharibifu wa mazingira hususani maeneo ya mazalia ya samaki. Katika tafiti iliyofanyika mwaka 2008 imeonyesha kuwa samaki katika Ziwa Victoria wanapungua kwa kasi kubwa. Katika Mkoa wa Kagera takwimu za samaki waliovuliwa zinadhihirisha wazi kupungua kwa samaki, mwaka 2006/2007 zilivuliwa tani 6,216.80, 2007/2008 tani 6,878.30 na mwaka 2008/2009 tani 5,995.01

 

Uchangiaji wa Sekta ya Uvuvi katika Uchumi

Sekta hii inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuinua hali ya uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na pia pato kwa Serikali kutokana na kodi mbalimbali. Katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2009 samaki waliovuliwa katika Mkoa wa Kagera
 
 

Uchangiaji wa Sekta ya Uvuvi katika ajira

Sekta ya Uvuvi katika Mkoa imetoa ajira rasmi na isiyo rasmi kwa wananchi wapatao 30,579 ambao wanapata kipato kutokana na Uvuvi. Kiwanda cha uchakataji Vic-Fish kimetoa ajira ya wafanyakazi 400, kati yao asilimia 40 ni wanawake, na Kagera Fish ambacho kimeajiri wafanyakazi 217 kati yao asilimia 15 ni wanawake. Watu wengine wanaojihusisha na uvuvi wa samaki na mazao yake ni 23,220. Aidha wafanyabiashara na wachuuzi ni 6,742.

 

 
 
Udhibiti Juu ya Uvuvi Haramu
 

Sheria ya uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na Kanuni yake ya mwaka 2005 inaelekeza matumizi endelevu ya zana bora za uvuvi. Hata hivyo kumekuwa na ukiukwaji wa sheria na kanuni za uvuvi. Ili kukabili tatizo hili Mkoa umekuwa ukichukua hatua zifuatazo

• Kushirikisha Halimashauri zote zenye shughuli za uvuvi katika udhibiti wa uvuvi haramu. Halmashauri hizo ni Muleba, Chato, Missenyi, Bukoba/Vijijini na Bukoba Manispaa. Wadau wengine wanaoshirikishwa ni Jeshi la Polisi, Mahakama, TAKUKURU na Idara ya Uhamiaji.

•Kuendelea kufanya doria dhidi ya Uvuvi haramu kwa kutumia sheria ya Uvuvi Na. 22 ya 2003 pamoja na Kanuni zake za 2005. Doria zimefanyika katika maeneo mbalimbali ziwani, mialoni na nchi kavu katika wilaya za Muleba, Chato, Missenyi, Bukoba/Vijijini na Bukoba Manispaa.

• Kuelimisha jamii kuhusu uvuvi haramu na athari zake kiuchumi na kiafya kupitia semina, mikutano ya hadhara na vyombo vya habari.

•  Kutunga sheria ndogo za Halmashauri za kutoa adhabu kwa wanaokiuka sheria za uvuvi

•  Kuwafikisha Mahakamani wote waliobainika kukiuka sheria na kanuni za uvuvi. Jumla ya watuhumiwa 268 wamekamatwa, kati yao 78 wamefikishwa Mahakamani na kesi 11 zinaendelea. Watuhumiwa 190 wamelipa compound faini na kuliingizia Taifa kiasi cha shilingi 12,145,000.00 .

•  Kufanya doria katika vituo vya ukaguzi katika mipaka ya Mkoa na nchi jirani ya Rwanda (Rusumo - Ngara), mpaka wa Burundi (Murusagamba –Biharamulo, Kabanga –Ngara), na mpaka wa Uganda (Kyaka, Kabindi) ili kudhibiti zana haramu kuingia Mkoani na mazao ya samaki kutoroshwa.

•  Kushirikiana na idara ya Mahakama katika muundo wa Mahakama za haraka/papo kwa papo (mobile court) ili kutoa hukumu za haraka. (kiambatanisho C kinaonyesha matokeo ya doria baada ya azimio la Kampala la kupambana na uvuvi haramu kuanzia tarehe 1 Octoba 2008 hadi 30 Novemba 2009.

 
 
 

Baadhi ya wananchi Mkoani Kagera wanaojihusisha na uuzaji wa samaki katika soko kuu Bukoba

 
 

MFUMO WA MASOKO YA SAMAKI

Wavuvi na wafanyabiashara halali wa sangara wanauhakika wa kupata soko la kuuza samaki na mazao yake, kama ifuatavyo .

• I. kuwepo viwanda viwili ambavyo ni VIC-Fish na Kagera Fish kumechangia, kuwawezesha wananchi kuwa na kipato kizuri na kuweza kuwainua kiuchumi.

• II. Kutoa kibali kwa wafanyabiashara wanaouza mazao ya samaki na dagaa nje ya nchi , kama vile Rwanda , DRC, Burundi , Uganda , Zambia , Malawi , Somalia na Jumuiya ya nchi za Ulaya.

• III. Kuwepo kwa matumizi makubwa ya samaki Mkoani na Tanzania kwa ujumla, hivyo soko la samaki lipo la kutosha.

Aidha wafanyabiashara wanaouza mazao ya samaki na dagaa nje ya nchi, hupatiwa vibali vya kuuza mazao hayo kihalali. Elimu ya kukopa inatolewa kwa wavuvi, na taasisi binafsi na huwakopesha, mfano taasisi ya FINKA, PRIDE, NMB bank, NBC bank, CRDB bank na POSTA bank, na KADETFU

UDHIBITI WA UBORA WA SAMAKI NA MASOKO

Kwa kuzingatia Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2005, kitengo cha udhibiti wa Ubora wa samaki na Masoko, kimeweza kusimamia viwango vya Ubora katika Viwanda vya Uchakataji wa Samaki ambavyo ni Kagera Fish na VICFISH. Ili minofu ya samaki iendelee kuuzwa katika soko la Kimataifa, ni lazima ubora uliopasishwa na Jumuiya ya Ulaya (EU) uweze kufikiwa, jukumu hili linafanikishwa na Kitengo cha Ubora wa Samaki na Masoko.

Katika nia ya kuimarisha na kuboresha mialo mradi wa kusimamia na kuendeleza Ziwa Victoria (LVFO), umejenga mialo minne ya kisasa ya kupokelea samaki; mialo hiyo ipo:

•  Igabiro – Bukoba vijijini

•  Nyamkazi – Bukoba Manispaa

•  Iramba - Wilaya ya Muleba

•  Katembe - Wilaya ya Muleba

 

 

 
 
Kikosi cha Doria-Uvuvi Mkoani Kagera kikiwa kimekamata nyavu zinazotumika katika uvuvi haramu
 
CHANGAMOTO KATIKA KUDHIBITI UVUVI HARAMU
 
  1. Jiografia ya Ziwa katika Mkoa wa Kagera ni ngumu na kuna mtawanyiko mkubwa wa mialo, hii inaleta ugumu katika kufika kwa wakati kutoka mwalo hadi mwalo .
  2. Mawasiliano ya simu yanasaidia hata hivyo pia yamechangia kudhoofisha juhudi za vyombo vya doria kwa kuwa wahalifu huwasiliana wao kwa wao mara wanapoviona vyombo hivyo katika zoezi la doria. Hii huchangia wavuvi haramu kukimbia baada ya kuficha nyavu zao haramu, au kufunga vibanda vyao na kukimbia.
  3. Uhaba wa bajeti katika Halmashauri husababisha doria za kudhibiti uvuvi haramu kutofanyika kwa ufanisi.
  4. Uhaba wa maafisa ugani na vitendea kazi katika Halmashauri huchangia doria ya kudhibiti uvuvi haramu kutofanyika kwa ufanisi.

 

 
 

MCHANGO WA ASASI NYINGINEZO

Taasisi zisizo za kiserikali (NGO's) kama vile ECO-LAB, LAV-NET na KADETFU zinashiriki kikamilifu katika uendelezaji na utunzaji wa sekta ya uvuvi kama ifuatavyo:

•  Kuwakopesha wajasiriamali wa sekta ya uvuvi zana endelevu za uvuvi,

•  Kutoa elimu ya ufugaji wa samaki katika mabwawa,

•  Uendelezaji na uanzishwaji wa mialo yenye sehemu zilizoboreshwa za kupokelea samaki (receiving point),

•  Kutoa elimu ya utunzaji mazingira na usafi wa mialo kwa kuwajengea vyoo vya mfano,

•  Kutafuta fedha na kushiriki maadhimisho ya siku ya wavuvi duniani.

 
 

UKUZAJI VIUMBE HAI WA MAJINI

Ukuzaji wa viumbe hai kwenye maji umejikita zaidi kwenye ufugaji wa samaki tu; hii ni kutokana na hali halisi ya Mkoa kuzungukwa na maji baridi. Sambamba na hali hiyo mazingira ya ufugaji wa samaki yanaruhusu, kwani kuna rutuba nzuri na uwepo wa maji kwa muda wote wa mwaka. Samaki wanaofaa kufugwa katika mabwawa kulingana na jiografia ya Mkoa ilivyo ni pamoja na samaki aina ya Tilapia na Clarius.

Hata hivyo jamii kubwa ya watu wa Mkoa wa Kagera wana mwitikio mdogo wa ufugaji wa samaki kuliko ufugaji mwingine wowote wa viumbe hai wa majini.

Takwimu zinaonesha kuwa Mkoa ulikuwa na mabwawa 360 mwaka 2007; mabwawa mengi yaliyokuwa yameanzishwa kipindi cha nyuma hayafanyi kazi kwa sasa, hii inatokana na kutokuwa na vifaranga bora vya samaki, na elimu duni juu ya uchimbaji na utunzaji wa mabwawa hayo kwa wakati huo.

Hivi sasa kuna uingizaji haramu wa samaki hai wanaotumika kama chambo katika uvuvi wa sangara aina ya kambale ( Clarius gariepinus ) ndani ya nchi yetu wakitokea nchi jirani ya Rwanda, Uganda na Burundi. Hii ni biashara inayowaingizia wadau fedha nyingi hivyo kufanya dhana ya utumiaji wa mabwawa yaliyochimbwa kupungua. Aidha ni hatari kwa suala la uingizaji wa magonjwa na pia kuua mbegu ya samaki wa asili wa nchi hii. Kambale hawa hutumiwa na wavuvi wa Sangara kama chambo (live bait)

MAFANIKIO KATIKA SEKTA YA VIUMBE HAI MAJINI.

Katika kipindi cha Oktoba 2008 hadi Novemba 2009 ufuatiliaji ulifanyika katika Halmashauri 7 na kubainisha yafuatayo

  1. Kuwepo kwa mabwawa 197 na wafugaji 1,341 ambao wameelimishwa juu ya ufugaji samaki,
  2. Kupandikizwa Idadi ya vifaranga 37,423 aina ya sato (rejea Jedwali Na.5), na samaki waliovunwa ni Kilogramu 5,500 aina ya Sato ambao walikuwa na thamani ya Tsh 1,100,000/=.
  3. kutolewa kwa vibali 8 vya kusafirisha vifaranga kwa kipindi hicho. Hii inatokana na mwamko mdogo wa wananchi katika kuelewa umuhimu wa kutumia vibali. Hata hivyo elimu itaendelea kutolewa kwa wananchi juu ya umuhimu wa kufuata utaratibu.
Kuchimba bwawa la mfano lenye ukubwa wa mita 10 kwa 10 katika Manispaa ya Bukoba, eneo la ofisi ya Doria Mkoa ambalo linatarajiwa kupandikizwa samaki aina ya Tilapia wapatao 20,000 katika kipindi cha mwaka 2009/2010. Bwawa hilo pia linatarajia kuwa la mfano kwa kuelimisha wafugaji na kutoa vifaranga kwa wafugaji wa samaki kimkoa

MIKAKATI YA KUENDELEZA NA KUSIMAMIA RASILIMALI YA UVUVI

Mkoa umejiwekea mikakati mbalimbali ya kuendeleza Sekta ya Uvuvi pamoja na udhibiti wa uvuvi haramu na uharibifu wa mazingira. Juhudi hizi zinafanywa kwa kuzingatia sheria ya uvuvi na kanuni zake.Mkoa utahakikisha panakuwepo utashi wa kisiasa katika ngazi zote ili kutekeleza Yafuatayo;

•  kuandaa mipango ya kila Halmashauri ya kudhibiti ongezeko la nguvu ya uvuvi kwa kutoa kiwango fulani cha idadi ya leseni ili kutunza rasilimali ya uvuvi.

•  Kuweka mikakati ya nyongeza ya ajira kwa maafisa ugani katika Halmashauri zote ili kuongeza idadi kutoka 26 walioko sasa hadi kufikia 56 ili kujaza mapengo yaliyopo katika upungufu wa maafisa ugani katika Halmashauri.

•  Kuendelea kutoa elimu ya madhara ya maambukizi ya ukimwi kwa wavuvi katika mialo,

•  Kuhakikisha Halmashauri zinashirikiana na BMU's kulinda rasilimali za uvuvi na ukusanyaji mapato yatokanayo na sekta ya uvuvi,

•  Kuhakikisha NGO's zinaendeleza juhudi za dhati kwa kutoa elimu, mikopo na uibuaji wa miradi mbadala ili kupunguza nguvu ya uvuvi na uvuvi haramu katika ziwa Victoria .

•  kuratibu ubainishaji wa wajasiriamali katika sekta ya uvuvi kwa kuwapa elimu ya ufugaji wa samaki katika Wilaya zote.

•  Kutoa msaada vijijini wa kuibua miradi ya ufugaji viumbe hai (samaki) ili miradi hiyo iingizwe kwenye Mipango ya Halmashauri ya Kuendeleza Kilimo na ufugaji (DADPS na DASIP).

•  Kushirikisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama katika kudhibiti wafanyabiashara wasiofuata sheria za uvuvi na kanuni zake.

•  Kuhamasisha wananchi kuchimba mabwawa ya kufugia samaki katika Wilaya zote.

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 

 

 
     
     
 
     
Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, BUKOBA, TEL: 028 - 2220215/17, FAX: 028-2222341