JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OFISI YA MKUU WA MKOA KAGERA
     
 
     
 
 
     
YANAYOTUHUSU
 
Kutuhusu [Anuani ] [ Nyumbani ] au
 
MAELEZO YA JUMLA KUHUSU MKOA
 

Mkoa wa Kagera unapatikana kaskazini magharibi mwa nchi ya Tanzania. Makao makuu ya mkoa yapo katika mji wa Bukoba umbali wa kilometa 1500 kutoka Dar es Salaam, mkoa huu unapakana na nchi ya Uganda kwa kaskazini, Rwanda na Burundi kwa upande wa magharibi mkoa wa Kigoma, Mwanza kwa upande wa kusini na ziwa Victoria kwa upande wa mashariki. Vile vile mkoa wa Kagera uko kusini mwa ikweta kati ya 1 “00” na 2”45” latitudi. Kwa Iongitudo uko katika nyuzi 30”25” na 32”40” Mashariki mwa ‘greenwich'.

Mkoa wa Kagera ulijulikana kama “Ziwa Magharibi” jina hili lilidumu katika kipindi cha ukoloni na baada ya uhuru mpaka mwaka 1979 baada ya vita kati ya Tanzania na Uganda.

Mkoa ulipata jina hili kutokana na mto Kagera ambao hutiririsha maji yake kutoka Rwanda kupitia kaskazini na kumwaga maji yake katika ziwa Victoria.

Mkoa wa Kagera una jumla ya eneo la kilomita za mraba 39,168 kati ya hizo kilometa za mraba 28,513 ni eneo la nchi kavu za kilomita 10,655 ni eneo la maji. Ukiacha mbali wilaya za Biharamulo na Chato ambazo ni tambarare sehemu kubwa ya mkoa ni yenye milima na vilima vilivyogawanywa na mabonde yenye matingatinga. Upande wa magharibi wa mkoa mito mingi inamwaga maji yale katika mto Kagera ambao nao humwaga maji yake katika ziwa Victoria.

 

Hali ya hewa

Hali ya hewa ya mkoa wa Kagera kwa ujumla ni ya joto la wastani wa 26.02 sentigredi. Mvua zinanyesha kwa wastani wa milimita 800-1,100 kwa mwaka kati ya mwezi Septemba na Januari na kati ya mwezi Machi na Mei. Mvua hizi ndizo zinazowezesha kuwepo kwauoto wa asili wa kuvutia katika maeneo mengi ya mkoa. Kwa miaka ya kawaida mkoa hupata mvua za uhakika za vuli na masika ambazo ni muhium kwa shughuli za kilimo na ufugaji.

 

UTAWALA

 

Wakati tunapata UHURU, mkoa wa Kagera ulikuwa na jumla ya wilaya nne (4), wilaya hizo ni Ngara ambayo ilianzishwa mwaka 1947, Biharamulo, Bukoba, na Karagwe mwaka 1958 ambayo ilizinduliwa rasmi na gavana wa kiingereza Sir Richard Turnbul. Aidha, mwaka 1975 wilaya mpya ya Muleba ilianzishwa kutoka kwenye wilaya ya Bukoba na mwaka 2007 wilaya ya Chato na Missenyi zilianzishwa na kuunda jumla ya wilaya 7 za mkoa wa Kagera.

Kwa sasa mkoa wa Kagera una jumla ya wilaya saba (7) na halmashauri 8. Wilaya hizo ni Bukoba, Muleba, Biharamulo, Ngara, Chato, Karagwe, Missenyi na Ngara. Halmashauri ni Bukoba Manispaa, halmashauri ya wilaya ya Bukoba, Muleba, Biharamulo, Ngara, Chato, Karagwe na Missenyi.

Kisiasa mkoa una jumla ya majimbo 10 ya uchaguzi (Muleba 2, Karagwe 2, Ngara 1, Biharamulo 1, Missenyi 1, Bukoba Manispaa 1, Bukoba Vijijini 1 na Chato jimbo 1).

 

IDADI YA WATU

 

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 1967 mkoa ulikuwa na watu 658,712, mwaka 1978 watu 1,009,379, mwaka 1988 mkoa ulikuwa na watu 1,326,183 na mwaka 2002 watu 2,033,888. Ongezeko la idadi ya watu lilikuwa kwa wastani wa asilimia 2.7. Aidha, mwaka 2011 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002 mkoa unakadiriwa kuwa na idadi ya watu 2,746,058.

 

 

Halmashauri Ya Wilaya

Idadi ya Watu

 

1978

1988

2002

MAOTEO 2011
Missenyi
-
-
-
174,889
 

Bukoba (V)

296,462

343,950

395,130

467,129

Bukoba (M)

36,914

47,009

81,221

153,016

Muleba

217,493

274,447

386,328

492,404

Chato
-
-
-
383,162
 

Biharamulo

165,580

209,524

410,794

252,218

Karagwe

185,013

292,589

425,476

542,517

Ngara

107,917

158,658

334,939

422,044

JUMLA

1,000,379

1,326,183

2,033,888

2,746,058

 

Chanzo: Ofisi Kuu ya Takwimu Taifa (NBS) , 2011

 

HISTORIA YA MKOA WA KAGERA

Mkoa huu haukuitwa Kagera bali ulikuwa moja ya maeneo yaliounda jimbo lililoitwa Lake Province. Jimbo hili lilijumuisha Wilaya ya Bukoba, Musoma, Shinyanga na Tabora. Baadaye ulibadilishwa jina na kuitwa ‘West Lake Region' (Ziwa Magharibi) na kujumuisha Wilaya 4 za Ngara, Biharamuro, Karagwe na Bukoba.

Kabla na baada ya kuja kwa wakoloni mkoa wa Kagera ulikuwa na utawala wa Kimila (Chiefdoms) uliogawanyika katika himaya 8. Himaya hizo ni pamoja na Kyamutwara, Kihanja (Kanazi), Kiziba, Ihangiro, Bugabo, Karagwe, Biharamulo (Rusubi) na Maruku (Bukara).

Baadhi ya Watemi waliotawala himaya hizo ni pamoja na Emmanuel Rukamba (Kyamtwara), Rumanyika (Karagwe), Kasusura (Biharamulo), Lugomola (Bukara), Rutinwa (Kiziba), Kayoza (Bugabo), Kahigi (Kihanja) na Nyarubamba (Ihangiro). Kila mtemi alikuwa na walinzi wake walioitwa Warugaruga.

Wakazi wa asili ya Kagera ni wabantu na wengi wao wana asili ya Bunyoro. Wanaongea lugha sawa na ile ya Wanyoro, Wanyankole, Watoro na Wakiga. Busubi na Bugufi wana lugha na desturi sawa na Watusi, Wahutu na Waha. Lakini makabila hayo ni ya Wabantu wa Ziwa (Interlacustrine Bantu) na yanafanana mila na desturi. Makundi hayo yaligawanyika kati ya wachungaji (Bahima) ambao walitawala na wakulima (Bairu) ambao walitawaliwa na mara nyingi kudharauliwa. Bahima (Balangira) walikuwa na koo chache zipatazo 20 na walitawaliwa na Wahinda, Wabito na Wankango.

Bairu walikuwa na Koo kama 130 zenye mashina 24 ambayo kiasili walikuwa Bairu lakini kwa kuoa katika Bahima au kufanya kazi kwa Watemi walipandishwa hadhi na kuwa Bahima (Batware). Kila ukoo uliitwa jina la Baba mwanzilishi wake na kina ukoo ulikuwa na kitu walichokatazwa kula (Omuziro) na mnyama walioshirikishwa nae (Ekyerumono).

Mkoa ulibadilishwa jina na kuitwa Kagera mwaka 1979 baada ya vita ya Tanzania na Uganda. Chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa aliyekuwepo wakati huo Capt. Peter Kafanabo jina la Kagera lilipendekezwa kwa sababu ya mto Kagera unaogusa sehemu kubwa ya Wilaya zote zinazounda Mkoa wa Kagera.

Uchumi wa wenyeji wa Kagera ulijikita katika mashamba ya migomba. Chakula chao kikuu ni ndizi katika aina zake mbalimbali. Katika mashamba yao hulima mazao mengine kufuatana na msimu. Mazao hayo ni pamoja na maharage, mihogo, mahindi na mboga. Baada ya kuja kwa wazungu waliongeza ulimaji wa kahawa kama zao la biashara lililowasaidia kujiongea kipato.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 
 
 
 
 

 

 
 
 
 
 

MAJIMBO YA UCHAGUZI

Mkoa unayo majimbo ya Uchaguzi 10 na wapo Wabunge 9 wa kuchaguliwa na Wabunge 3 wa viti maalum. Jumla ya Wabunge 11 wanatoka chama cha Mapinduzi (CCM) na Mbunge 1 anatoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo. Majina ya waheshimiwa wabunge na majimbo wanayowakilisha pamoja na wale wa viti maalumu ni kama ifuatavyo:-

 

 

Na

Jina La Mbunge

Jimbo

Chama

Wilaya

1.

Mhe. Hamis Sued Kagasheki

Bukoba Mjini

CCM

Bukoba

2.

Mhe. Jason Samson Rweikiza

Bukoba Vijijini

CCM

Bukoba

3.

Mhe. John Pombe Magufuli

Chato

CCM

Chato

4.

Mh. Dk Antony Mbasa  

B'mulo Magharibi

CHADEMA

Biharamulo

5.

Mhe. Begumisa Gosbert Blandes

Karagwe

CCM

Karagwe

6.

Mhe. Eustace Katagira

Kyerwa

CCM

Karagwe

7.

Mhe. Anna Tibaijuka

Muleba Kusini

CCM

Muleba

8.

Mhe. Charles Mwijage

Muleba Kaskazini

CCM

Muleba

9.

Mhe.Asumpta Nshunju Mushama

Nkenge

CCM

Missenyi

10.

Mhe. Deogratius Ntukamazina

Ngara

CCM

Ngara

11.

Mhe. Bernadetha Mushashu

Viti Maalumu

CCM

12.

Mhe. Elizabeth Batenga

Viti Maalum

CCM

13.

Mhe. Conjester Rwamulaza

Viti Maalum

CHADEMA

 

Vyama vya siasa vinavyoendesha shuguli zake vizuri hapa mkoani ni pamoja na CCM, TLP, NCCR - Mageuzi, CUF, UMD, UDP, na CHADEMA. Hatuna matukio ya kukiukwa kwa sheria na utaratibu kwa vyama vya siasa.

 

HALI YA UCHUMI NA MAENDELEO YA MKOA

Uchumi wa mkoa unategemea zaidi kilimo ambapo zaidi ya asilimia 70 ya watu wanajishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara. Shughuli za uvuvi, mifugo,viwanda na madini zinachangia pia katika uchumi wa mkoa.

Kwa kuzingatia malengo ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA) , Dira ya Taifa ya mwaka 2025 na malengo ya Milenia, Mkoa wa Kagera unaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo na umepiga hatua katika sekta za uchumi, miundo mbinu na huduma za jamii. Hata hivyo pamoja na hatua hizi zilizopigwa, juhudi za wananchi mkoani za kujiletea maendeleo zinakumbana na matatizo na vikwazo mbalimbali ambavyo vimeendelea kupatiwa ufumbuzi kwenye mipango ya maendeleo ya Mkoa.

 

KANDA ZA IKOLOJIA (ECOLOGICAL ZONES) :

Mkoa wa Kagera umetenganishwa katika Kanda tano za kilimo kuzingatia mwinuko wa maeneo hayo kutoka usawa wa bahari na kiwango cha unyeshaji wa mvua.

 

Ukanda wa kwanza : Ukanda huu unajumuisha maeneo ya mashariki ya wilaya ya Bukoba na Muleba yanayoambaa kandokando ya ziwa victoria na uko katika mwinuko wa mita 1,300 mpaka 1,500 kutoka usawa wa bahari. Mvua zinanyesha kwa wastani wa milimita 800 - 1,750 kwa mwaka. Shughuli kuu za kiuchumi katika eneo hili ni kilimo cha ndizi, maharagwe, mahindi na kahawa. Eneo la ukanda huu ni asilimia 17 ya eneo la Mkoa.

 
 
 

Ukanda wa pili : Huu ni ukanda wa juu ulioko kwenye mwinuko wa mita 1,400 mpaka 1,800 kutoka usawa wa bahari. Ukanda huu unajumuisha maeneo ya juu ya wilaya ya Karagwe na Ngara na mvua zinanyesha kwa wastani wa milimita 800-1,000 kwa mwaka. Mazao yanayolimwa kwenye ukanda huu ni ndizi, maharagwe, mahindi na kahawa. Eneo la ukanda huu ni asilimia 19 ya eneo la mkoa.

 

 

Ukanda wa Tatu : Ukanda huu uko katika mwinuko wa mita 1,000 kutoka usawa wa bahari na unajumuisha wilaya ya Ngara ,Biharamulo na Chato.Mvua zinanyesha kwa wastani wa milimita 750-800 kwa mwaka. Shughuli kuu za kiuchumi ni uzalishaji wa mazao ya mahindi, mihogo, mpunga, mtama, karanga na pamba. Eneo la ukanda huu ni asilimia 27 ya eneo la mkoa.

Ukanda wa Nne : Ukanda huu upo kwenye mwinuko wa mita 1,000 kutoa usawa wa bahari na unajumuisha maeneo ya mashariki ya wilaya ya Karagwe,wilaya ya Misenyi na maeneo ya magharibi ya wilaya ya Bukoba. Mvua zinanyesha kwa wastani wa milimita 800-1,000 kwa mwaka. Shughuli kuu za kiuchumi ni kilimo cha mazao ya mahindi,maharagwe na ufugaji. Eneo la ukanda huu ni asilimia 10 ya eneo la mkoa.

 Ukanda wa Tano :Ukanda huu unajumuisha maeneo ya kaskazini ya wilaya ya Karagwe na Misenyi na uko kwenye mwinuko wa mita 1,000 kutoka usawa wa bahari .Ukanda huu unapata mvua za wastani wa milimita 750-800 kwa mwaka.Sehemu kubwa ya ukanda huu ni misitu ya hifadhi na mapori ya akiba. Eneo la ukanda huu ni asilimia 27 ya eneo la mkoa.

 

 

 

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
     
     
 
     
Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, BUKOBA, TEL: 028 - 2220215/17, FAX: 028-2222341