Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Mohammed A. Babu amehitimisha sherehe za Wakulima za Nane Nane 2011 Mkoani Kagera zilizofanyika katika uwanja wa maonesho ya wakulima wa Kyakailabwa nje kidogo ya mji wa Bukoba tarehe 8/8/2011.
Maonesho hayo ya Nane Nane yalizinduliwa tarehe 01/08/2011 na kuhitimishwa tarehe 8/8/2011. Maonesho hayo yalihusisha shughuli mbalimbali za kilimo kwa wakulima pamoja na taasisi mbalimbali binafsi na za serikali zinazojishughulisha na kilimo kuonyesha shughuli zake kwa wananchi kwa lengo la kuwaelimisha wananchi uzalishaji wa mazao yenye tija katika maeneo yao.
Katika kuhitimisha sherehe za Nane Nane 2011 Mhe. Babu pamoja na kutembelea mabanda mbalimbali ya maonyesho pia aliweza kuwahutubia wananchi waliofurika katika uwanja wa Kyakailabwa juu ya sherehe za Nane Nane pamoja na masuala mbalimbali yanayoukabili mkoa wa Kagera hususan changamoto za kilimo.
Mhe. Babu katika hotuba yake alisisitiza sana wananchi kuelimishwa kupitia Halmashauri zao juu ya “KILIMO KWANZA” na nguzo 10 za kilimo kwanza. Mhe. Babu alisema kuwa wananchi walio wengi hawajui maana ya dhana ya kilimo kwanza na nguzo zake 10 jambo ambalo linawafanya wengi wao kutoelewa kilimo kwanza ni nini. Kama wananchi wataelewa maana ya kilimo kwanza wataweza kulima kilimo chenye tija kwa kutumia mbolea, kuacha jembe la mkono na kuzingatia kanuni za kilimo bora.
Mhe. Babu aliwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya zote za mkoa wa Kagera na Manispaa kuwaelimisha wananchi juu ya ufugaji wa samaki katika mabwawa pamoja ufugaji wa nyuki kwenye mizinga. Wananchi wakiweza kuelimishwa vizuri juu ya ufugaji wa samaki katika mabwawa na nyuki wataweza kujipatia kipato cha haraka na kuinua kipato chao kwa siku. Mhe. Babu alitoa mfano kuwa mzinga mmoja wa nyuki unaweza kumpatia mwananchi Tshs 160,000/= kila mara baada ya miezi mitatu.
Masuala Mtambuka; Aidha katika hotuba yake Mhe. Babu alisisitiza na kutoa angalizo kwa masuala mtambuka ambayo ni changamoto ndani ya mkoa wa Kagera. Masuala hayo ni ushirika, uhaba wa chakula, upandaji wa bei ya sukari, mafuta ya petrol, taa na dizeli, kuhifadhi mazingira na miaka 50 ya uhuru.
Ushirika, Mhe. Babu aliwahimiza wananchi kuendelea kujiunga katika ushirika ili kupata maendeleo ya haraka. Mkijiunga katika ushirika ni rahisi kupata mikopo yenye riba nafuu pia kupata misaada kwa urahisi kuliko mtu mmoja mmoja. Aidha Mhe. Babu aliipongeza Kagera Co operative Union (KCU1990 LTD) kwa kupandisha bei ya kahawa mpaka 1300/= kwa kilo moja ya kahawa ya robusta ya maganda pia pamba imepanda bei mwaka huu kutoka 500/= -550/= mwaka jana na kufilia 800/= kwa kilo moja mwaka huu.
Uhaba wa Chakula, Mkuu wa Mkoa alisema kuwa Kagera ni mkoa mmojawapo kati ya mikoa 16 inayokabiliwa na uhaba wa chakula Tanzania. Wilaya zilizoathirika ni Wilaya ya Muleba na Chato ingawa kwa Chato tathmini inaendelea kufanyika. Serikali ilitoa tani 2076 za mahindi ya chakula na Tshs 256,000,000/= za kusomba mahindi hayo mpaka Wilayani Muleba.
Mhe. Babu aliwatahadhalisha wananchi wa mkoa wa Kagera kutumia chakula walicho nacho kwa uangalifu mkubwa maana hali ya chakula nchini si nzuri. Mhe. Babu aliwaagiza viongozi wote wa serikali kuendelea kupambana na wafanyabiashara wote wanaovusha chakula nje ya nchi na kuwachukulia hatua za kisheria pale wanaobainika kukiuka amri ya kutovusha chakula nje ya nchi.
Upandaji wa bei ya sukari, akitoa ufafanuzi wa kupanda bei ya sukari, Mhe. Babu alisema, sukari inatakiwa kuuzwa kwa Tshs 1700/= kwa kilo moja. Lakini sukari imekuwa ikipandishwa hadi kufikia 2500/= kwa kilo moja kutokana na nchi jirani sukari kuuzwa kwa bei ya juu sana jambo linalowafanya wafanyabiashara wadogowadogo kuwauzia sukaria wafanyabiashara wakubwa toka nchi jirani na kupata faida kubwa.
Pia jambo lingine linalosababisha upandaji wa sukari ni pale viwanda vinaposimamisha uvunaji wa miwa kuanzia kipindi cha masika mpaka mwezi Julai linapunguza uzalishaji wa sukari. Mhe. Babu aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwabaini wafanyabiashara wanaouza sukari zaidi ya 1700/= ili serikali iwachukuliwe hatua za kisheria.
Mafuta ya petroli, taa na dizeli, kutokana na serikali kutoa bei elekezi za kuuza mafuta baadhi ya wafanyabiashara wa mafuta wamefunga vituo vya kutolea huduma ya mafuta na kuwafanya wananchi kukosa huduma hiyo. Mhe. Babu alitoa ufafanuzi kuwa kwa mfanyabiashara yeyote hapa mkoani atakayegundulika kufunga kituo cha mafuta cha kutolea huduma atachukuliwa hatua mara moja ikiwa ni pamoja na kunyanganywa leseni. Aidha mafuta yanatakiwa kuuzwa kwa bei elekezi zilizotolewa na serikali.
Kuhifadhi Mazingira, hivi sasa kutokana na uchafuzi mkubwa wa mzingira duniani yamekuwepo mabadiliko makubwa ya tabia nchi jambo linalosababisha matetemeko ya ardhi, vimbunga vingi na mvua za kupindukia mara kwa mara. Kutokana na hayo yote Mhe. Babu alisisitiza wananchi kuendelea kutunza mazingira ili kuepukana na madhara ya uharibifu wa mazingira.
Miaka 50 ya Uhuru, Mkuu wa Mkoa aliwakumbusha wananchi kuwa mwaka huu Tanzania inatimiza miaka 50 ya uhuru, kwahiyo katika kuadhimisha sherehe hizo wananchi wote wanakumbushwa kushiriki kuanzia ngazi ya Kitongoji, Kijiji, Kata, Tarafa, Wilaya mpaka ngazi ya Mkoa.
Katika Kuhitimisha sherehe za Nane Nane 2011 Wilaya ya Missenyi iliweza kujinyakulia kombe kama ishara ya ushindi wa jumla katika maonyesho ya 2011. Pia Missenyi iliweza kuziongoza Wilaya zote za Mkoa wa Kagera na kupata zawadi ya kwanza kwa upande wa Wilaya. Vilevile Wilaya ya Missenyi imeweza kunufaika zaidi na maonyesho ya Nane Nane 2011 kwa Kikundi cha Ujasilia mali cha Wakulima Tumaini SACOSS kunufaika na fedha mbegu zaidi ya milioni 900/= kutoka benki ya CRDB .

|